Friday, March 22

Mgomo wa daladala watikisa Morogoro, Moshi

0


Moshi/Morogoro. Wakazi wa Morogoro na Moshi mkoani Kilimanjaro jana walionja adha ya usafiri kufuatia mgomo wa daladala na baadhi yao kulazimika kufanya safari kwa kukodi bodaboda, teksi na kutembea kwa miguu.

Mjini Moshi, mgomo wa daladala ambako hadi jana saa 12 jioni kulikuwa na hali ya sintofahamu ulitokana na madereva wa daladala maarufu ‘Hiace’ kupinga Bajaj kupakia abiria katika vituo vya mabasi.

Katika Manispaa ya Morogoro, daladala zinazofanya safari zake kati ya Kihonda-Mjini ziligoma kutoa huduma ya usafiri kwa takribani saa moja kwa madai ya kutozwa ushuru wa Sh1,000 katika stendi ya Msamvu na Sh 1,000 wanapoingia standi ndogo ya mjini kati.

Katika taratibu za kuzima mgomo huo madereva 12 walikamatwa na polisi huku viongozi watatu wa chama cha madereva wa manispaa wakikamatwa na baadaye kuachiwa.

Wakizungumzia mgomo mjini Moshi, madereva wa daladala walisema mgogoro kati yao na wenye Bajaj ni wa tangu 2013 lakini viongozi wameshindwa kuutatua.

“Bajaj zinaingia katika maeneo yetu ya biashara na kupakia abiria. Mgogoro huu tumeupeleka katika ngazi mbalimbali lakini hakuna ufumbuzi. Tumeamua kugoma leo ili muafaka upatikane,” alisema Jackson Kinyaiya.

Dereva mwingine wa daladala, Sanael Mushi aliungana na Kinyaiya na kubainisha kuwa baadhi ya viongozi wana maslahi na jambo hilo na ndio sababu wanashindwa kulimaliza.

Dereva mwingine, Hussein Ally alisema haoni faida ya kazi wanayoifanya kwa kuwa imeingiliwa na Bajaj, hivyo ameamua kurejesha funguo za daladala kwa mwajiri wake kwa kuwa hakuna anachokipata.

Akizungumzia sababu za mgomo huo, ofisa mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoani Kilimanjaro, John Makwale alisema chanzo ni Bajaji kutozingatia sheria na kufanya kazi za daladala.

Alisema kila dereva anatakiwa kutoa huduma kwa mujibu wa leseni yake la sivyo sheria itachukua mkondo wake.

“Maelekezo ambayo tumeyatoa leo (jana) tumewataka watu wa Bajaj na daladala watoe huduma kwa mujibu wa leseni zao. Sisi tutaendelea kusimamia sheria na atakayeenda kinyume tutamchukulia hatua. Bajaj wasiingilie maeneo ya daladala,” alisema Makwale.

Mratibu wa Bajaji Mkoa wa Kilimanjaro, Rashid Omary aliwataka madereva wa Bajaj kufuata sheria na kila mtu kukaa eneo lake kutokana na leseni yake inavyomtaka.

Mjini Morogoro madereva wa daladala walifunga lango la stendi hiyo ya Msamvu wakidai kuwa uongozi wa stendi hiyo umekuwa ukiwalazimisha kutoa ushuru huo wakati kipato chao ni kidogo.

Agizo la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa kuwapa dakika 20 madereva hao kuondoa daladala zilizokuwa zimeziba barabara, lilitekelezwa na usafiri kurejea kama awali.

“Tumerudi barabarani tunaendelea na kutoa huduma baada ya kamanda wa polisi kututaka turudi na katuhakikishia kuwa kutafanyika mazungumzo. Ukweli ni kuwa fedha tunayotoa ni kubwa kulingana na kipato tunachokipata kwa siku,” alisema Mohamed Salehe.

Meneja wa Msamvu, Stanley Mhapa alisema anashangazwa na mgomo huo kwa kuwa walikubaliana namna nzuri ya kulipa ushuru huo ikiwemo kushusha abiria nje ya stendi ya msamvu.

Share.

About Author

Leave A Reply