Sunday, May 26

Mdau Yanga aipa ubingwa Simba Mapema

0


By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Wakati kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera akiwa hajakata tamaa ya ubingwa msimu huu, uenda hii ikawa habari mbaya kwake baada ya shabiki kindaki ndaki wa timu hiyo na mchambuzi wa soka nchini, Keny Mwaisabula kuitabiria ubingwa Simba

Simba yenye pointi 85 inahitaji ushindi katika mechi mbili kati ya nne ilizobakisha ili itetee ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu unaoelekea ukingoni.

Hata hivyo, timu hiyo inapewa presha na Yanga ambayo ina pointi 83 na michezo miwili mkononi, huku kocha Zahera akiamini bado wana nafasi ya kutwaa ubingwa.

Wakati kocha Zahera akiamini hivyo, Mwaisabula amesema sio kazi nyepesi kwa Yanga kumvua Simba ubingwa msimu huu.

“Nafasi ya ubingwa Yanga ilikuwa kwenye FA (Shirikisho), lakini wakaipoteza, kwenye Ligi sio rahisi,” alisema Mwaisabula na kufafanua.

“Msimu huu pamoja na kwamba baadhi ya wana Yanga wanaamini ubingwa bado, lakini tukubali tukatae sio rahisi kama tunavyofikiria,” alisema.

Mwaisabula ambaye alijitambulisha kama shabiki wa Yanga alisema licha ya kuipenda timu hiyo, lakini kwenye ukweli atasema.

“Simba inahitaji pointi tano ili kutangaza ubingwa, Yanga yenyewe inahitaji kushinda mechi zake mbili zilizosalia wakati huo huo ikisikilizia matokeo ya Simba ambayo ina mechi nne mkononi.

“Tukubali kwamba ubingwa tumeukosa na tujipange kwa ajili ya msimu ujao, maana kwa kikosi cha Simba, hamasa ya mashabiki, uimara wa uongozi, sidhani kama Simba inaweza kufungwa mechi tatu mfululizo au kutoa sare, haiwezekani,” alisema Mwaisabula.

S:Endapo Yanga itashinda michezo yake yote iliyosalia itafikisha pointi 89 wakati Simba yenyewe ikishinda mechi zake zilizosalia itafikisha pointi 97 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kwenye Ligi Kuu.


Share.

About Author

Leave A Reply