Saturday, August 24

Mbwa wenye kichaa wakatisha maisha ya watoto wawili

0


By Lilian Lucas, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Watoto, Sara Nalentino (9) mkazi wa Kologoso na Mohamed Iddi (8) mkazi wa mtaa wa Msamvu Kata ya Kihonda Magorofani, wamefariki dunia baada ya kung’atwa na mbwa wenye kichaa.

Kaimu Ofisa Afya Manispaa ya Morogoro, Prisca Gallet akizungumza na mwandishi wa Mwananchi Leo Jumatano Mei 22,2019 ofisini kwake, amesema matukio ya vifo hivyo yalitokea kwa nyakati tofauti baada ya kufikishwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Gallet amesema Sara aling’atwa na mbwa Aprili 4, 2019 na alipofikishwa hospitali alitibiwa vidonda na mama yake mzazi alipewa maelekezo ya kumpeleka kupata chanjo, lakini hakutekeleza na kubaki nyumbani.

Amesema ilipofika Mei 20, mtoto huyo alianza kuonyesha dalili za kichaa cha mbwa na kupelekwa hospitali na Mei 21 alifariki dunia.

Akizungumzia kifo cha Mohamed, amesema  aling’atwa na mbwa Machi 3, 2019 na hakufikishwa hospitali kupatiwa chanjo na alipopata dalili za kichaa cha mbwa ndipo alipelekwa hospitali, lakini alifariki dunia Machi 4, 2019.

Gallet amesema pamoja na idara ya afya kutoa elimu ya juu ya chanjo pindi mtu anapoumwa na mbwa mwenye kichaa, bado wananchi wengi hawazingatii na kuwaacha wagonjwa nyumbani.

“Ugonjwa wa kichaa cha mbwa hauna tiba, wananchi wanapoona mtu ameng’atwa na  mbwa wanatakiwa kuwahi kutoa taarifa, changamoto kubwa iliyopo ni mbwa wengi kutolindwa na wenye mifugo hiyo na hivyo kuzagaa mitaani,” amesema.

Amesema katika kipindi cha Januari  hadi Mei, 2019, wagonjwa 168 wameripotiwa kung’atwa na mbwa wanaume wakiwa 97 na wanawake 71 na vifo viwili.

Aidha, amesema kwa manispaa ya Morogoro vituo vinavyohusika na chanjo ni uhuru maarufu kama Nunge, Sabasaba, na Kingolwira hivyo wananchi ni vyema kwa sasa kutumia vituo hivyo na kwamba, kwa sasa kumekuwa gharama ya uchangiaji ambayo ni Sh30,000 kwa dozi moja na kwa mgonjwa ni dozi tano ambayo ni Sh150,000.

Amesema dalili za kichaa cha mbwa ni kuogopa mwanga, kuogopa maji, kushindwa kula na kuwa na tabia isiyo ya kawaida ikiwa ni pamoja na kung’ata kila anachokiona mbele yake.

“Huu ugonjwa unaweza kukuchukua mwezi mmoja ama sita ama mwaka na inategemea umeng’atwa eneo gani,” amesema.

Ofisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Morogoro, Mohamed Chamzhim amesema wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali ikiwamo ya kutengeneza mitego kwa ajili ya kuwakamata mbwa ambao wengi wao wamekithiri maeneo ya mijini.

Chamzhim amesema kipindi cha Januari hadi Mei, mbwa 24 walikamatwa na akasita (6) kwa kutumia mitego miwili iliyopo na kwamba, wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.

“Tukumbuke kufuga mbwa ni hiyari ila kuhudumia ni jukumu la mfugaji, hivyo ni vyema wafugaji wakafuata taratibu zilizopo kwa kumfungia mbwa na kuwafungulia katika muda unaotakiwa,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply