Wednesday, August 21

Mbunge wa CCM awataka upinzani kukumbuka maneno ya Rais Kikwete

0


By Ibrahim Yamola, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma ameishauri Serikali kuwapuuza wanaopinga mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge na kuwataka wapinzani kuikumbuka kauli ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Akizungumza wakati wa mjadala wa bajeti ya Nishati kwa mwaka 2019/2020 leo Jumanne Mei 28, 2019 bungeni Jijini Dodoma, amesema amekuwa akiwasikiliza wabunge wa upinzani wanavyoupinga wakati ukweli ni kwamba, ni mradi wenye tija kwa Taifa.

“Nimekaa hapa miaka miwili nawasikiliza, Rais wa awamu ya nne (Jakaya Kikwete) aliwahi kusema akili za kuambiwa, changanya na za kwako…mabeberu wamekuwa wakikataa mradi huu, sasa msiingie mkenge wa kuwaunga mkono.

“Mradi huu una faida kubwa sana, faida ya kwanza tunakwenda kupata umeme kwa bei ndogo na mwingi wenye uhakika,” amesema Vuma.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kuzalisha mpunga utakaopatikana kule na utakwenda kurusha Afrika Mashariki, “lakini itakuwa kama kivutio na mimi naamini mradi huu hauwezi kuharibu mazingira bali kutunza mazingira.

“Tunajua matumizi ya kuni yatapungua na huu utakuwa ni utunzaji wa mazingira na si uharibifu wa mazingira,” amesema.

“Hili jambo lina baraka za Bunge na mwaka jana tulipitisha bajeti ya Sh700 bilioni na imani yangu, fedha zilitolewa na Serikali itekeleze mradi huu isiogope miluzi na wanaopinga ni wa kuwapuuza tu,” ameongeza.

Naye Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya amesema Wakala wa Nishati vijijini (Rea) awamu ya tatu, inakwenda taratibu sana licha ya waziri kwenda vijijini, akitoka tu hali inarudi kulekule, jimboni kwangu ni vijiji saba tu, kwa kasi hii tutaweza kumaliza na kila siku vikwazo haviishi.

“Utasikia wanasema tatizo ni nyanya, nyaya zikija wanasema ni nguvu, zikija wanatoa sababu zingine. Yaani umeme Kaliua imekuwa ni tatizo na kila siku tunakosa umeme saa 6 kwa siku.

“Kama umeme hakuna ina maana saluni hazifanyi kazi, mashine hazifanyi kazi, viwanda vidogo haviwezi kuzalisha na leo kuanzia saa moja hadi saa 8 hakukuwa na umeme, umeme ni maendeleo, umeme ni uchumi na kama umeme haupo, utawezaje kufikia maendeleo ,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply