Saturday, July 20

Mbunge: Mawaziri hawafanyi kazi bali wanazilinda

0


Dodoma. Mbunge wa Momba (Chadema) David Silinde amesema mawaziri wamekuwa wakilinda nafasi zao kwa kusifia na si kwa kufanya kazi.

Akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka wa fedha 2019/20 bungeni leo Novemba 6 2018, Silinde amesema mpango huo haujaweka mkakati wa namna gani unaweza kutekelezwa.

Amesema nchi kama Rwanda kabla ya kupewa uongozi, watu wamekuwa wanapewa mkataba wa ufanisi ambapo  kiongozi akishindwa moja kwa moja anaondolewa katika uongozi.

“Unasema mimi nikiwa Waziri wa Fedha na Mipango ninaeleza nitafanya nini (Rwanda)? Ukishindwa kutekeleza unaondoka ‘automatically’ hakuna mjadala. Sasa humu ndani unakuta mtu analinda uwaziri kwa kusifia si kwa kufanya kazi,”amesema.

“Tukiwapima mawaziri bungeni sisi wenyewe tunajua waziri gani ni porojo? Hapa nani anamdanganya Rais. Tunawajua  wote hapa mlivyo. Mtu anayejua kusifia sana ndio anaonekana kuwa anajua kufanya kazi tunaliangamiza Taifa hili.”

Amehoji kuwa inakuaje Serikali inaandika katika kitabu cha mpango moja ya mafanikio ni kulipa madeni kama kwamba walivyokopa walikuwa hawajui kuwa ni lazima watalipa.

“Unakuta mtu anaandika huduma za maji kuwa miradi 1,595 ya maji vijijini imekamilika na imekuwa ikihudumia watu milioni 30 huu ni uongo uliotukuka. Kila mbunge analalamika shida ya maji humu ndani,”amesema.

Amesema Rais wa Rwanda ameunda bodi ya ushauri ambayo inawajumuisha marais wastaafu wa nchi nyingine duniani pamoja na watendaji wakuu wa mashirika duniani.

Amesema kuwa katika nchi hiyo hakuna mradi ambao unatekelezwa bila kupitiwa na wahandisi washauri mara tatu.

Share.

About Author

Leave A Reply