Tuesday, July 23

Mbunge aeleza mateso wanayopata wananchi wa Kigoma

0


Dodoma. Sakata la vifo vya wananchi mkoani Kigoma katika mgogoro wa ardhi limeendelea kuchukua sura nyingine na limeibuka bungeni.

Sakata hilo ndilo lililopelekea Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kushikiliwa kwa siku tatu polisi jijini Dar es Salaam kwa madai ya uchochezi.

Leo Jumanne Novemba 6, 2018, bungeni Mbunge Viti Maalumu, Josephine Genzabuke (CCM) ameliibua sakata hilo akisema wananchi wanaumizwa na wanateswa kwa kupigwa na kunyanyaswa na kunyang’anywa baiskeli zao na pikipiki.

Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo alihoji kama Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wanapingana na agizo la Rais John Magufuli lililotaka wananchi wa maeneo ya Kagera Nkanda waendelee kulima bila kuongeza maeneo.

“Hawa TFS wanaua watu, wanatoboa nyayo za watu, wanawakata mikono na kuwatesa, ni kwa nini wanafanya hivyo wakati Rais aliagiza wasibughuziwe,” alihoji Genzabuke.

Hata hivyo, Spika Job Ndugai alimzuia Mbunge huyo kuendelea na swali lake akisema mambo anayozungumza ni mazito hivyo akamkatisha na kumtaka akae chini licha ya kutaka aendelee kulijenga swali lake lakini akaitwa Mbunge mwingine.

Baadaye Ndugai alisimama na kutoa ufafanuzi kwa kukemea maswali anayosema ni mazito ambayo yalipaswa kupelekwa kwa Waziri Mkuu siyo kuuliza swali la nyongeza.

“Lakini Kasulu (Kigoma) kuna wabunge wengi mbona hawakusimama, angalieni wabunge katika kauli zenu maana tukisema lipelekwe kamati ya maadili itakuwa shida,” alisema Ndugai.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga alikiri kuwa Rais aliagiza Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kigoma kuwapimia wananchi eneo hilo.

Alisema jumla ya hekta 10,012.61 zilitengwa kwa ajili ya kilimo kwa wananchi wa maeneo hayo na kijiji cha Mvinza kilipewa hekta 2,174, Kagerankanda 2,496 na eneo jingine hekta 5,342.61 zilitengwa kwa ajili ya matumizi mengine ya wananchi.

Share.

About Author

Leave A Reply