Tuesday, July 23

Mbegu za GMO zinavyoweza kuwaepusha wakulima na viuatilifu

0


Mahindi ni zao linalolimwa kwa wingi nchini kwa matumizi ya chakula na biashara. Ni zao linalochukua asilimia 45 ya eneo lote linalolimwa nchini.

Hata hivyo, zao la mahindi liki hatarini kutokana na uvamizi wa magonjwa na wadudu waharibifu hasa viwavi jeshi vamizi (Fall Armyworms).

Hayo ndiyo machungu yanayowakuta wakulika katika kijiji cha Nyamwilimilwa Wilaya ya Geita Vijijini mkoani Geita walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari wakisema wameshindwa kufikia malengo yao ya kilimo cha biashara.

Edward Faustin ambaye ni mkulima mwezeshaji katika kijiji hicho anasema alitarajia kuvuna magunia 25 kwenye shamba lake la ekari mbili, lakini kwa wadudu hao ameishia kupata magunia manne tu.

“Hawa wadudu kwa mara ya kwanza nimeanza kuwaona mwaka 2016 baada ya kuanza kulima hili shamba.

Awali sikukagua shamba hili kwa sababu sikuelewa kwa kumbe inatakiwa kulikagua shamba wiki mbili kabla ya kuanza kulima,” alisema Faustine.

Alisema kwa sasa hawana uwezo wa kununua viuatilifu badala yake wamekuwa wakitumia njia za kienyeji ikiwa pamoja na kuweka majivu kwenye mahindi bila mafanikio.

Mkulima mwingine kutoka kijiji cha Ntinechi kata ya Nyamilimwilwa Tizi Buhicho anasema licha ya kuanza kulima kilimo cha kisasa, magonjwa yamekatisha ndoto yake ya mafanikio.

“Tatizo ni wadudu wanaoshambulia mahindi. Tulishazoea kulima mashamba makubwa ili tupate mazazo mengi, lakini ilikuwa inatugharibu sana, tukawa tunapata mazao kidogo,” anasema.

“Tumetumia dawa za kubuni za kienyeji, kwa mfano mimi nilitumia mafuta ya ng’ombe nayachemsha na kukoroga na kumwagia kila hindi ili zile siafu zifuate yule mdudu ndani, lakini ilishindikana. Awali tulitegemea kufanya kilimo cha biashara lakini tumeishia kupata mzao machache ya kula tu.”

Maelezo kama hayo ameyatoa Elias Lusinge Kilingwa mkazi wa kijiji cha Nyamilimilwa akisema wadudu aina ya viwavi jeshi vimewasumbua kwa karibu miaka 10 sasa.

Ofisa ugani wa kijiji cha Nyamwilimilwa, Samuel Kisika anasema tatizo la viwavi jeshi litawaathiri wakazi wa kijiji hicho na mkoa kwa ujumla.

Kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakitumia gharama kubwa kununua viuatilifu ili kukabiliana na wadudu waharibifu.

Licha ya kuwa na gharama kubwa, upulizaji wa dawa shambani hupoteza muda mwingi na ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.

Uhandisi jeni (GMO) suluhisho la wadudu waharibifu

Wakati wakulima wakitumia gharama kubwa kupuliza viuatilifu kwenye mashamba yao, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) katika kituo cha Makutopora wanaendelea na utafiti wa uhandisi jeni katika mahindi.

Uhandisi jeni ni uhamishaji wa jeni (vinasaba) kutoka kwa kiumbe hai kimoja na kupandikiza katika kiumbe hai kingine ili kupata sifa zinazohitajika.

Kiumbe kilichofanyiwa mabadiliko ya jeni kwa lugha ya kigeni huitwa genetically modified organism (GMO).

Mpaka sasa Tanzania inafanya utafiti wa GMO kwa mbegu za muhogo katika kituo cha utafiti wa kilimo cha Mikocheni (Mari) Dar es Salaam na mbegu ya mahindi katika kituo cha utafiti wa kilimo cha Makutopora.

Mahindi ya GMO

Utafiti wa mahindi ulianza tangu mwaka 2016 kwa njia ya kawaida (conventional method) ambayo hufanyika kwa kuchanganya mbegu tofauti ili kupata mbegu bora.

Tayari mbegu zilishazalishwa na zinatumiwa na wakulima.

Utafiti wa GMO ulioanza mwaka 2017 bado unaendelea katika kituo hicho.

Mtafiti wa mahindi kutoka kituo cha utafiti cha Ilonga, Justin Ringo anasema jaribio la mahindi linaloendelea kituoni hapo linahusu ukinzani dhidi ya ukame wa wastani na wadudu aina ya bungua, ambapo mahindi yalipandwa kati ya Agosti 16 na 17, 2018

Akifafanua jinsi wanavyofanya utafiti kwa mashambulizi ya wadudu, Ringo anasema kuna funza 20 wa bungua wa mahindi waliwekwa katika kila mche wa mhindi mara mbili (wiki ya tatu na ya tano baada ya kupanda).

Jaribio lingine lilihusisha mahindi yaliyopuliziwa viuaadudu mara saba ili kudhibiti uharibifu wa wadudu ambapo anasema tathmini ya kiasi cha uharibifu uliofanywa na wadudu ulifanyika Oktoba 1 na 2 ambazo ni sawa na wiki ya saba baada ya kupanda.

“Tathmini inaonesha kuwa mahindi ya GMO yameweza kustahimili mashambulizi ya bungua na viwavijeshi vamizi kwa kiasi kikubwa sana ukilinganisha na mahindi yasiyokuwa ya GMO,” anasema Ringo.

Anaendelea, “Kiwango cha mashambulizi ya mahindi ya GMO kilikuwa kinafanana na kiwango kilichoonyeshwa na mahindi yaliyopuliziwa dawa ya kuuwa wadudu mara.”

Anasema mahindi hayo yamewekewa vinasaba viwili; kimoja kikiwa kinakinga wadudu na kingine kinaongeza uvumilivu wa ukame.

Akifafanua kuhusu vinasaba hivyo, Ringo anasema vinatokana na bakteria waliovunwa kutoka ardhini ambao hawana madhara kwa binadamu.

Share.

About Author

Leave A Reply