Sunday, August 25

Mawaziri Malawi, Tanzania waagizwa kushughulikia changamoto za maendeleo

0


By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais John Magufuli na mwenzake wa Malawi, Arthur Peter Mutharika, wamewaagiza mawaziri wa nchi zote mbili kushughulikia haraka changamoto zinazosababishwa kusuasua kwa shughuli za kiuchumi ikiwamo biashara na miradi ya maendeleo.

Viongozi hao wametoa maagizo hayo jana Jumatano Aprili 24, 2019 katika Ikulu ya Lilongwe nchini Malawi katika siku ya kwanza ya ziara rasmi ya kikazi ya siku mbili anayoifanya Rais Magufuli.

Baadhi ya maeneo ambayo mawaziri wameagizwa kushughulikia haraka ni kuharakisha ujenzi wa kituo cha huduma za pamoja za mpakani (One Stop Border Post – OSBP) katika mpaka wa Kasumulu, kuharakisha utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya utalii.

Maagizo mengine ni kuhusu usafiri wa anga na kutatua changamoto zinazokikabili kituo cha mizigo cha malawi (Malawi Cargo Center Ltd).

Pia, marais wote wawili wamekubaliana kutafuta mkopo nafuu wa fedha kwa ajili ya kutekeleza kwa pamoja mradi wa bonde la Mto Songwe ambao utazalisha megawati 180 za umeme zitakazotumika kuendelea viwanda na matumizi mengine ya kijamii.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa Tanzania na Malawi zina kila sababu ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo kwa kukuza uchumi wa nchi hizo, kuimarisha ustawi wa jamii na kukuza zaidi biashara ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa ambako biashara kati ya nchi hizo ina thamani ndogo ya Sh146.112 bilioni iliyorekodiwa mwaka 2018.

Ameongeza kuwa Tanzania kwa upande wake imeendelea kuweka juhudi kubwa za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwamo kuimarisha bandari hasa za Dar es Salaam na Mtwara, kujenga bandari kavu na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mbambabay ambayo itawawezesha wafanyabiashara wa Malawi kuitumia kwa umbali mfupi wa kilomita 820.

“Tumeamua kuimarisha bandari ya Mtwara ili kuiwezesha kupitisha tani milioni moja kwa mwaka ikilinganishwa na tani 400,000 za sasa, tunakamilisha ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay ili ndugu zetu wa Malawi msilazimike kupitisha mizigo yenu Dar es Salaam, kwa hiyo natoa wito kwenu kuwa baada ya mwaka mmoja anzeni kutumia bandari ya Mtwara,” amesema Magufuli.

Katika mazungumzo hayo amempa pole Rais Mutharika na wananchi wote wa Malawi kwa kupoteza ndugu zao na wengine kupata majeraha kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai, amewatakia heri katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao.

Naye Rais Mutharika amemshukuru Rais Magufuli kwa kuamua kufanya ziara yake ya kwanza nchini Malawi kwa nchi za Kusini mwa Afrika, amempongeza kwa juhudi kubwa za kufanya mabadiliko ya kiuchumi nchini Tanzania.

Pia, amemshukuru kwa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi vilivyotolewa na Tanzania kwa waathirika wa mafuriko ya Kimbunga Idai, na amemshukuru kwa kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ubalozi wa Malawi katika Jiji la Dodoma nchini Tanzania.

Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe mama Janeth,  amewasili mjini Lilongwe jana asubuhi na baada ya mapokezi rasmi ameweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa Malawi, hayati  Profesa Bingu Wa Mutharika uliopo katika viwanja vya Bunge.

Katika mapokezi hayo Mutharika ameongozana na mkewe mama Getrude, baadaye jana jioni Rais Magufuli alishiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake katika Ikulu ya Kamuzu mjini Lilongwe

Share.

About Author

Leave A Reply