Monday, March 18

MAWAIDHA YA IJUMAA: Kuumbika kwa mwanadamu katika Qur’an na sayansi

0


Kama kuna swali muhimu kwa mwanadamu ni nini chanzo changu? Kabla ya Qur’an, wanadamu waliamini mtoto hutokana na damu ya hedhi ya mwanamke na wengine wakiamini anatokana na manii ya mwanamume.

Huo ndiyo ulikuwa msimamo rasmi wa Wagiriki na Warumi na ulidumu kwa karne nyingi hadi karne ya 18 wakiamini kwamba mbegu ya uzazi ya baba au ile ya mama ilikuwa na kiumbe mdogo ambaye ndiye anakuja kuwa mtoto ndani ya fuko la uzazi.

Kuumbika kama huku kwa mwanadamu kulijulikana kisayansi kama ‘preformation theory’ au nadharia ya kuumbika kwanza dhidi ya ile iliyokuweko tangu enzi za mwanafalsafa wa Kigiriki aitwaye Aristotle.

Wakati hayo yakiendelea, Qur’an ilikuwa imeshaelezea vizuri kwamba mwanadamu huumbika kutokana na mbegu ya uzazi ya mama na ile ya baba katika Sura ya 76 iliyopewa jina la “Mwanadamu” (Insaan) aya ya 2.

“Hakika sisi tumemuumba mwanadamu kutokana na mbegu ya uzazi ya baba na mama ili tumtie majaribuni na tukamjaalia kuwa ni mwenye kusikia mwenye kuona”.

Katika aya nyingine iliyoko katika Sura ya 75 aya ya 37-39: “Hivi mwanadamu anadhani ataachwa tu hivi hivi (asimtii Mola wake)? Hivi hakuwa mbegu ya uzazi iliyotonwa itokanayo na manii? Kisha akawa kitu chenye kuning’inia akamuumba na akamsawazisha? Na akamfanya kuwa jinsi mbili, ya kiume na ya kike?

Tunajifunza nini katika aya hizi?

Aya hizi zinatufahamisha kwamba mwanadamu ameumbika hatua kwa hatua mbegu ya uzazi hadi kuwa kiumbe kamili.

Katika aya ya ya 2 ya Sura ya 76, neno haswa lililotumika kuelezea uhakika huu wa kisayansi ni “Nutfatun Amshaajin” yaani chembe hai ya uzazi iliyochanganyika. Maana yake ni kwamba mwanadamu ameumbika kwa chembe ya uzazi iliyochanganyika. Tunachojifunza hapa ni kwamba;-

Mosi, mwanadamu ameumbika kutokana na chembe mbili za uzazi, moja kutoka kwa baba na nyingine kutoka kwa mama.

Mbili, mwanadamu ameumbwa ili atiwe majaribuni yaani katik amaisha yake hapa duniani mwanadamu yuko katika chumba cha mtihani na kila mtu anao mtihani wake na muda wake wa kuufanya ambao ni umri wake tangu awe na utambuzi.

Tatu, Qur’an inataja kwanza mlango wa fahamu wa kusikia kabla ya ule wa kuona kama dalili kwamba kichanga kikiwa tumboni huanza kusikia wakati kuona huja baada ya kuzaliwa.

Nne, mwanadamu hupitia hatua za ukuaji kuanzia mbegu ya uzazi ya baba au mama iitwayo Nutfah (reproductive cell) kisha mbegu ya uzazi inayoundwa na kuchanganyika kwa mbegu ya uzazi ya baba na ile ya mama ndani ya fuko la uzazi la mama kutoka Nutfatun Amshaajin (Zygote).

Tano, kisha baada ya Nutfatun Amshaajin mwanadamu huingia katika hatua ijulikanayo kama Alaqah neno la Kiarabu ambalo hutafsiriwa kama kitu chenye kuning’inia au tone la damu.

Katika sura ya 24 aya ya 12-14, Qur’an inaelezea hatua kamili za uumbaji wa mwanadamu kuanzia hatua uumbaji wa asili kwa udongo kisha uumbaji ndani ya fuko la uzazi la mama Nutfah hadi kuwa kiumbe kamili kwa maneno haya:

“Na kwa hakika tumemuumba mwanadamu kutokana tope la udongo wa mfinyanzi, kisha tukaifanya Nutfah katika ngome madhubuti (mji wa mimba). Kisha tukaiiumba Nutfah kuwa Alaqah kisha tukaifanya Alaqah Mudhghah kisha tukaifanya Mudhghah mifupa kisha kukaivika mifupa nyama kisha tukambadilisha kuwa kiumbe mweingine, basi ametakasika Mwenyezi Mungu mbora wa kuumba”.

Mshangao wa Wanasayansi kuhusu misamiati ya Qur’an

Misamiati iliyotumika katika Qur’an inaelezea kwa karibu mno hakika za kisayansi ambazo hazikuwa zikijulikana kabla ya uvumbuzi wa darubini zenye nguvu kubwa mnamo karne ya 19. Neno Alaqah ambalo mara nyingi limetafsiriwa kama tone la damu pia lina maana ya kitu chenye kuning’inia. Neno hili halikutumika hapa kwa bahati mbaya bali linaendana na umbile halisi la kiini tete kikiwa katika mji wa mimba wa mama.

Katika hatua ya Alaqah, kiini tete huonekana kama tone la damu kutokana na vishipa vidogo vidogo vya damu (blood capillaries) na katika hatua hii, kiini tete hujing’ang’aniza katika kuta za mji wa mimba kwa juu hivyo kuwa kama kitu kilichoning’inia.

Dr Keith Moore, ambaye ni bingwa wa masuala ya hatua za ukuaji wa mwanadamu katika mji wa mimba nchini Canada aliwahi kunukuliwa akisema

“At first I was astonished by the accuracy of the statements that were recorded in the 7th century AD, before the science of embryology was established”,

Tafsiri: “Kwanza nilishangazwa na usahihi wa maneno yaliyorekodiwa karne ya saba kabla ya sayansi ya ukuaji wa kiini tete haijaanzishwa” (Keith L. Moore and Abdul-Majid A. Zindani, The Developing Human with Islamic Edition). Hatua hizi za ukuaji wa mwanadamu kama zilivyoelezwa katika Qur’an ni sehemu ya muujiza wa Qur’an na uthibitisho kwamba Qur’an kweli ilitoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu Mtume Muhammad (S.A.W) hakuwa akijua kusoma wala kuandika.

Itoshe kusema kwamba hizi ndiyo hatua za uumbaji na ukuaji wa mwanadamu ndani ya mji wa mimba wa mama. Kuzijua hatua hizi humfanya mwanadamu awe mtiifu kwa Mola wake na kwa wazazi wake.

Toleo lijalo, tutakwenda mbele na kuangalia ni nini lengo la mwanadamu kuwepo duniani? Nani amjulishe mwanadamu kuhusu lengo hilo?

Share.

About Author

Leave A Reply