Tuesday, July 23

Maujanja na jeuri yote ya Yanga kumbe yapo hapa tu

0


By CHARITY JAMES

Dar es Salaam.KABLA Ligi Kuu Bara 2018-2019 haijaanza, hakuna aliyeitilia maanani Yanga. Wengi waliamini kuwa, kama ilivyomaliza msimu uliopita ndivyo itakavyoanza msimu mpya.

Hata katika klabu zilizokuwa zikitabiriwa kwenye mbio za ubingwa, Yanga haikuwamo kwa sababu ya hali mbaya ya kiuchumi na aina ya wachezaji iliyokuwa imewasajili, huku ikitoka kufanya vibaya msimu uliopita kiasi cha kutema taji lao.

Hata hivyo unaambiwa mpaka sasa ligi ikiwa imeingia raundi ya 14, Yanga ipo kivingine kabisa na inazitetemesha klabu zilizokuwa zikipigiwa chapuo kubeba taji msimu huu.

Yanga i[po nafasi ya tatu katika msimamo nyuma ya Azam na watetezi Simba, lakini ikiwa ni moja ya timu mbili ambazo hazijaonja machungu ya kufungwa hadi sasa ikiwa na alama 26 kwa kucheza mechi 10 tu ikishinda nane na sare mbili.

Wababe hao wameshinda mechi dhidi ya Mtibwa Sugar (mabao 2-1), Stand United (4-3), Coastal Union (1-0), Singida United (2-0), Mbao FC (2-0), Alliance (3-0), KMC (1-0) na Lipuli  (1-0). Imetoka suluhu na Simba na sare ya 1-1 dhidi ya Ndanda katika mechi yao ya mwisho iliyopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Je, unajua kinachowapa jeuri mabingwa hao wa kihistoria wa soka nchini? Wala usikonde Mwanaspoti inabainisha mambo kadhaa yaliyopo nyuma ya mafanikio hayo ya Yanga katika msimu huu unaoshirikisha klabu 20.

Kocha Mkongo, Mwinyi Zahera amehusika kwa kiasi kikubwa kuimarisha Yanga kuanzia kwenye safu ya ulinzi, kiungo hadi eneo la ushambuliaji ambalo bado lina changamoto kwani hakuna straika tegemeo wa kufunga mabao muhimu.

Zahera ni muumini wa soka la kushambulia linalotegemea zaidi eneo la kiungo na ukiitizama Yanga kwenye michezo 10 iliyocheza eneo hilo limechangja matokeo waliyonayo kwa kiasi kikubwa.

Mkongomani huyo, anapenda kutumia viungo wawili wakali wenye utulivu na sio kuishia kukaba tu ndio maana, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekuwa akifiti kwa kufanya vizuri kwenye eneo hilo huku kwa mbali Papy Kabamba Tshishimbi akiendelea kuingia kwenye mfumo huo.

Mara kadhaa Tshishimbi amekuwa akipigiwa  kelele za kuangaika uwanjani kitu ambacho kinaweza kumchosha kwa haraka lakini taratibu amekuwa akibadilika.

Ibrahimu Ajibu ‘Kadabra’ amekuwa akicheza  mbele ya viungo hao wakabaji kwa madhumuni ya

kutengeneza nafasi za mabao cha ziada anachokitoa Kadabra ni uwezo wake wa kufunga.

Yanga imekutana na wepesi wa kucheza michezo yao mingi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, hiyo ikiwa ni moja ya sababu zinazowabeba mpaka sasa wakiwa nafasi ya tatu katika msimamo.

 Mashabiki wake wamepata  jeuri kimtindo na kuwasahaulisha kuwa timu yao bado ipo kwenye kipindi cha mpito kiuchumi.

Aina ya soka la Yanga la pasi fupi na ndefu kwenye eneo la kiungo hutegemea ubora wa kiwanja na ukiangia idadi ya mechi zao zote 10  zimechezewa taifa.

Hapo tukipigia hesabu na mechi ambazo walikuwa ugenini, lakini kidizaini ni kama walikuwa nyumbani mfano mechi dhidi ya Simba na KMC ambazo zilichezwa pia Uwanja wa Taifa.

Yanga imekuwa na hali ya utulivu na mshikamano tangu iondokewe na Mwenyekiti wao, Yusuf Manji aliyejiuzulu Mei 20, mwaka jana.

Kuanzia wanachama, viongozi hadi mashabiki wamekuwa kitu kimoja katika kila jambo, kiasi kwamba huwezi kuamini kama Yanga hii ndio iliyopoteza ubabe wake kiuchumi.

Ukitaka kujua Yanga ya sasa ni moja, angalia harambee iliyokuwa ikiendeshwa ili kuisaidia timu fedha, namna wanachama mashabiki na wadau wa klabu hiyo walivyojitolea kuichangia na kuifanya Yanga iwe imara kama ilivyo sasa.

Hata zile kelele za migomo baridi ya wachezaji, imesahaulika kwa sababu Yanga imekuwa ikifanya mambo yake kama mchwa na kuifanya iwe imara zaidi na ndio maana imekuwa ikipata matokeo yanayoonekana yamechangiwa na kila mmoja.

Yanga wako nyuma mchezo mmoja ukilinganisha na watani zao wa Simba wanaolingana nao pointi kwa sasa ila wakitofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa. Pia wapo nyuma kwa michezo miwili dhidi ya vinara, Azam wenye alama 30, nne tofauti na walizonazo Yanga.

Tofauti ya pointi ni mdogo baina ya Yanga na Simba na Azam wanaojiita Jeshi la Korea Kaskazini, inawapa jeuri Jangwani wakiamini kuwa wakifanya vyema katika mechi zao basi watakaa kileleni.

Yanga imeshaweka  wazi mipango yao ya dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa wiki ijayo (Nov 15) ambapo Kocha Zahera amesema amepanga kuongeza nyota wanne hatari kwenye kikosi chake cha sasa

asicghotaka kukibadilika sana.

Zahera anasema lengo ni kuimarisha timu yake kuanzia kwenye eneo la beki, kiungo, winga na ushambuliaji ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwa sasa.Baadhi ya nyota wanaotajwa kufanya mazungumzo na Yanga ni kiungo wa Mounana, Guylain Kisombe Makuntima anayecheza soka la kulipwa Gabon, nyota huyo mkataba wake unamalizika mwezi huu hivyo atakuwa huru kujiunga Yanga.

Licha ya Yanga kuonekana kutulia na kufanya mambo yao kwa raha zao, bado wana kibarua kigumu baada ya kucheza mechi karibu zote jijini Dar es Salaam.

Presha ya sasa ya Yanga ni ndogo kutokana na matokeo mazuri ambayo wameyapata kwenye michezo 10 ya mwanzo kwa sababu ya morali ya ushindi, hata hivyo ni lazina ijiandae kisaikolojia kwa safari zao za mikoani.

Mechi hizo ikianza kucheza viporo vyake viwili mfululizo mara baada ya timu ya taifa, Taifa Stars kurejea toka Lesotho ilipoenda kucheza mchezo wao wa Kundi L kuwania Fainali za Afcon 2019.

Yanga itaenda kanda ya Ziwa kuanzia Nov 21 kwa kuvaana na Mwadui, kabla ya kuifuata Kagera Sugar, bila kukaza msuli yanaweza kujikutwa wakitibuliwa rekodi yao ya kutopoteza mchezo hata mmoja ikiwa sambamba na Azam.

Share.

About Author

Leave A Reply