Sunday, August 25

Masele: Kusimamia haki si utovu wa nidhamu

0


By Ibrahim Yamola, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele amesema kusimamia misingi ya haki za binadamu asitafsiriwe kuwa ni mtovu wa nidhamu.

Alisema hayo jana baada ya kutoka katika mahojiano na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu tuhuma za utovu wa nidhamu.

Masele ambaye pia ni makamu wa kwanza wa rais wa Bunge la Afrika (PAP) alihojiwa kwa zaidi ya saa nne kuanzia saa 5.34 asubuhi hadi saa 9.18 alasiri na kamati hiyo inayongozwa na mwenyekiti wake, Emmanuel Mwakasaka.

Baada ya mahojiano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa jengo la utawala bungeni, Masele alisema anaamini kamati itamtendea haki huku Mwenyekiti Mwakasaka akisema baada ya kumaliza kumhoji na kupitia mahojiano hayo Watanzania watajuzwa.

Kamati hiyo ilimhoji Masele ikitekeleza agizo la Spika Job Ndugai alilolitoa Mei 16 alipolitangazia Bunge akimtuhumu mbunge huyo kwa utovu wa nidhamu na kumtaka kurejea nchini kutoka Afrika Kusini alikokuwa akiendelea na vikao vya PAP.

Hata hivyo, Masele aliendelea kuhudhuria vikao hivyo hadi vilipomalizika Ijumaa iliyopita.

Ndugai alimtuhumu Masele kuwa ni “kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya hovyohovyo na ndio maana tumemwita kidogo kwenye Kamati ya Maadili (ili) atufafanuliwe, huenda labda yuko sahihi, lakini kwa mtazamo wetu amekuwa akifanya mambo ambayo ni hatari.”

Ndugai alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni kugonganisha mihimili ya nchi.

“Anapeleka kwenye mhimili wa Serikali juu kabisa, maneno mengi ya uongo na ushahidi upo. Ni kiongozi ambaye amejisahau, hajui hata anatafuta kitu gani, ukiacha hizo vurugu ambazo hivi sasa zinaendelea kwenye Bunge ambalo analiongoza, ni kubwa. Hizo hazituhusu.”

Pamoja na kamati hiyo ya Bunge pia Spika Ndugai alielekeza Masele kuhojiwa na kamati ya maadili ya wabunge wa CCM. Hata hivyo, Masele alilieleza Mwananchi jana kwamba hajapata wito wa kamati hiyo na wala hajui tuhuma zake.

Baada ya kumaliza kuhojiwa, Masele alizungumza na waandishi wa habari akisema, “Mimi nina heshimu sana viongozi wangu, nimelelewa vizuri na wazazi, nimelelewa vizuri na chama changu, nimetokea umoja wa vijana kuanzia ngazi ya chini kabisa mpaka ngazi ya kitaifa kuwa mjumbe wa baraza kuu taifa, nimekuwa mbunge hii awamu ya pili.”

“Nimekuwa naibu waziri katika Serikali (ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete), natambua miiko ya uongozi, sijawahi kukurupuka, fuatilia rekodi zangu, chochote ninachokisema ninasimamia haki, ukweli na ninaheshimu viongozi wenzangu,” alisema.

Akizungumza kwa kujiamini, Masele alisema, “ni matarajio yangu haki itatendeka na mimi sijafanya jambo lolote kinyume na taratibu, kwenye kazi zangu ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na pia Bunge la Afrika kama makamu wa rais.”

Masele alisema, “nimekuwa nafanya kazi zangu kwa weledi, sijawahi hata siku moja, hata siku moja hata kuonywa tu kuwa nimefanya kosa lolote, ninajitambua, ninajitambua na ninajua ninachokifanya.”

Kuhusu utovu wa nidhamu alisema, “nawahakikishia Watanzania, nilichokuwa nasimamia ni misingi ya haki za binadamu na kufanya hivyo nisitafasiriwe ni utovu wa nidhamu.”

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mwakasaka alisema wamemaliza kumhoji mbunge huyo na kinachofuata ni kupitia mahojiano hayo na mara watakapomaliza watawasilisha taarifa yao kwa Spika Ndugai.

Alivyoingia bungeni, kamati

Masele aliwasili katika viwanja vya Bunge saa 3:40 asubuhi akiwa ameongozana na Mbunge wa Ileje (CCM), Janeth Mbene.

Mita takribani 70 kabla ya wawili hao kulifikia lango la kuingia bungeni, mtumishi wa Bunge alimsimamisha na kumpa kitabu cha kusaini. Alisaini na kuingia bungeni.

Masele hakukaa sana kwani dakika tano baadaye alitoka kwenda jengo la utawala yalikofanyika mahojiano.

Hiyo ilikuwa saa 4.53 asubuhi, hata hivyo mara baada ya kuingia wajumbe walikuwa hawajafika hivyo alitoka na kwenda katika mgahawa wa Bunge ambako alikaa karibu saa moja akizungumza na wabunge mbalimbali akiwamo Andrew Chenge.

Kuna wakati alitoka nje ya kuonekana akizungumza na mbobezi wa masuala ya sheria nchini ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge ambao waliteta karibu dakika saba.

Akiwa kwenye viwanja Bunge, Masele alikuwa akisalimiana na watu mbalimbali na Mwananchi lililokuwa karibu lilisikia wengine wakimwambia, ‘Mungu akusaidie

Saa 5.29 asubuhi, Masele akiwa amevalia kibegi chake cha mgongono alichoingia nacho pia bungeni, alikwenda katika jengo la utawala tayari kujibu tuhuma zinazomkabili ambapo mara baada ya kuingia ukumbini, walimtoa kwanza nje na ilipofika saa 5.34 asubuhi aliitwa tayari kuanza kujitetea.

Ilipofika saa 7.42 mchana, Masele alitoka na kwenda msalani kisha akarejea tena kuendelea na mahojiano saa 7.44 mchana ambapo alikaa hadi saa 9.18 alasiri alipotoka.

Share.

About Author

Leave A Reply