Wednesday, August 21

Mara Paap! Chelsea mikononi kwa Hazard Mabingwa Ulaya

0


LONDON, ENGLAND.ILE pyee kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Chelsea hao hapo mikononi mwa Eden Hazard.
Ni hivi, Chelsea itakuwa kwenye chungu namba moja kwenye upangaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Jambo hilo linaiweka kwenye hatari kubwa ya kumkabili staa wake Eden Hazard, kama atajiunga na Real Madrid.
Chelsea ya Kocha Maurizio Sarri imekamatia tiketi hiyo ya kuwa kwenye chungu namba moja cha upangaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa 4-1 Arsenal kwenye Europa League.
Kwa utaratibu huo, Chelsea itapangwa chungu kimoja na Manchester City, Barcelona, Paris Saint-Germain na Bayern Munich. Lakini, Chelsea haitakuwa kwenye hatari ya kumenyana na mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu ambapo anaweza kuwa Liverpool au Tottenham.
Lakini inawezekana kwa kikosi hicho cha Sarri kupangwa pamoja na Real Madrid ya Kocha Zinedine Zidane, ambayo msimu ujao moja ya mastaa wake kikosinni anaweza kuwa fundi wa mpira, Hazard.
Miamba hiyo ya Hispania, Los Blancos itakuwa kwenye chungu cha pili na wakali kama Atletico Madrid, Borussia Dortmund na mshindi wa pili kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Kutokana na hilo Chelsea inaweza kupangwa dhidi ya Hazard msimu ujao kama atakamilisha uhamisho wake wa kwenda kujiunga na wababe hao wa Bernabeu.
Akizungumza baada ya fainali ya Europa League, Hazard alisema: “Nadhani hii ni kwa heri, lakini kwenye soka huwezi kujua.
“Ndoto zangu zilikuwa kucheza kwenye Ligi Kuu England na nimefanya hivyo kwa miaka saba katika moja ya klabu kubwa kabisa duniani. Sasa ni muda wa kutafuta changamoto mpya.”
Imeelezwa Real Madrid ina uhakika wa kuinasa saini ya Hazard, ambaye ataigharimu Pauni 115 milioni, huku akiripotiwa kusaini mkataba wenye thamani ya Pauni 400,000 kwa wiki.


Share.

About Author

Leave A Reply