Sunday, August 25

MAONI: Ya Serengeti Boys yasijirudie kwa Taifa Stars katika fainali ya Misri

0


FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa mwaka 2019 inatarajiwa kufanyika nchini Misri kati ya Juni 21-Julai 19 ambapo nchi 24 zinatarajiwa kuonyeshana kazi kuwania taji hilo la Afrika.

Tanzania kwa mara ya nyingine tangu mwaka 1980 tuliposhiriki kwa mara ya kwanza, itakuwa miongoni mwa timu shiriki za fainali hizo za 32, ikipangwa Kundi C na nchi za Senegal, Algeria na Kenya.

Ratiba inaonyesha Taifa Stars itakata upete wa michuano hiyo kwa kuvaana na Senegal kabla ya kuumana na Kenya kisha kumalizana na Algeria.

Kama Stars itafanya vyema kwenye mechi zake tatu, itakuwa na nafasi ya kucheza hatua ya pili ya fainali hizo yaani 16 Bora kwa ajili ya kusaka timu nane za kuingia robo fainali.

Hatua hizo za juu ni ndoto za kila shabiki wa soka nchini na hata wachezaji na Kocha Mkuu wa Timu hiyo, Emmanuel Amunike wanatamani kuiona timu yao ikifika katika hatua hiyo na kuandika rekodi mpya, kwani Tanzania iliposhiriki mara ya kwanza ilitolewa hatua ya makundi tena ikiwa mkiani.

Tanzania ilimaliza ikikusanya alama moja tu ilitokana na sare ya 1-1 dhidi ya Ivory Coast, huku ikipoteza kwa wenyeji kwa kufungwa mabao 3-1 na Misri kwa 2-1 na kurudi nchini kusaka tiketi nyingine kwa miaka 39 na hatimaye kuipata mwaka huu wa 2019.

Kufuzu kwa Tanzania baada ya kuifunga Uganda imekuwa furaha kubwa kwa mashabiki wa soka kwa vile kiu ya kusubiri kuiona Stars ikienda katika fainali za Afcon zimechukua muda mrefu mno. Ilichosha.

Hata hivyo baada ya juhudi kubwa hatimaye Stars imeenda na sasa Watanzania wanajiandaa kukaa kwenye sebule zao kuangalia vijana wao wakifanya mambo mbele ya nyota wa kimataifa wa nchi za Senegal, Algeria na majirani wa Kenya.

Kwa kuwa imeshafahamika Tanzania imefuzu fainali izo na imepangwa kundi lipi, ni wakati wa kuanza kujipanga kwa maandalizi mazuri ili Stars isiende kuaibika na kuwa kichwa cha mwendawazimu mbele ya wapinzani wa kundi lao.

Muda uliosalia ni mchache mno kabla ya fainali hizo, hivyo ni muhimu kama Stars ikaitwa mapema na kuanza maandalizi kwa kucheza mechi kadhaa za kujipuima nguvu na nchi ambazo zinaweza kuwa kipimo kizuri kwao kabla ya safari ya Misri.

Ni kweli Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la FA hapa nchini bado inaendelea na hata kwenye nchi ambazo baadhi ya nyota wanaounda Stars nako ligi na michuano yao mbalimbali inaendelea hivyo kumuwia vigumu Kocha Amunike kupata wasaa wa kuita timu kwa sasa ili kuanza maandalizi.

Lakini kwa kuwa Tanzania inaenda kwenye fainali ngumu zinazohitaji kuwa na wachezaji ambao hawatakuwa wa majaribio ama mazoea, ni lazima kipindi hiki Kocha Amunike afuatilie kwa ukaribu baadhi ya mechi za Ligi Kuu ili kuona kama atapata nyota wapya ya kuimarisha kikosi chake.

Asiendelee kukariri kwamba fulani na fulani ni lazima wawe Stars na wataenda Misri, kuna baadhi yao waliokuwa wakiipigania Stars mpaka kufika fainali hizo, labda wameshuka viwango na kuna nyota wapya wanaendelea kufanya mambo na kuhitajika kwenda kulipigania taifa nchini Misri.

Hivyo ni nafasi ya Amunike kufuatilia wachezaji wanaofanya vizuri katika ligi na michezo mingine ndani na nje ya nchi ili kuona kama wanahitajika kuwepo Stars na kuwaita wakijumuika na wale ambao wamezoeleka kikosini.

Fainali hizo ni za kutengeneza heshima ya soka la Tanzania, lazima Stars iende na kikosi cha nguvu na kitakahimili vishindo vya nyota wenzao wa nchi shiriki kuanzia kundini mwao hadi wengine ambao huenda wakakutana nao kama watafanya vyema mechi za makundi.

Kadhalika katika kipindi hiki ndiko ambako wadau wa soka wanapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha Stars imara inaenda kuiwakilisha vyema nchi. Tujifunze kutokana na timu ya taifa ya vijana U17, Serengeti Boys ambayo haikuangaliwa kivile na kuandaliwa kwa ajili ya fainali za Afcon U17 2019 na mwishowe kujikuta wakiaibishwa licha ya kuwa wenyeji wa fainali hizo.

Kama Stars itaenda Misri ikiwa na maandalizi ya zima moto na uteuzi wa kikosi cha mazoea, basi tujiandae mapema kushuhudia aibu nyingine kwenye fainali za Afcon kama tulizopata Afcon U17 kwa Serengeti kuondoshwa michuanoni mapema na aibu ya kubugizwa mabao 12 katika mechi tatu.

Katika soka hakuna njia ya mkato ina ni maandalizi na kuwajenga wachezaji mapema ili kuhakikisha wanaenda kupambana wakiwa wa moyo wa kizalendo, huku wakitambua kuwa nyuma yao kuna Watanzania zaidi ya Milioni 50 wanawategemea katika kuwapa faraja na furaha kupitia fainali hizo.

Kwenye fainali kama hizo huwa hakuna muda wa kupoteza mara michuano ikianza, ni tofauti na hatua ya mchujo ambapo kama timu inapoteza mchezo inapata wasaa wa muda mrefu kujipanga kwa ajili ya mechi inayofuata.

Share.

About Author

Leave A Reply