Sunday, August 18

MAONI: Kampeni mifuko plastiki ni yetu sote

0


Sasa ni dhahiri kuwa siku chache zijazo Tanzania itaondokana na matumizi ya vifungashio vya plastiki.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ameshatangaza kuwa Juni Mosi itakuwa ndio mwisho wa uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki, hivyo wazalishaji na wananchi kwa jumla wajiandae kwa matumizi ya vifungashio mbadala.

Kwa msukumo wa Waziri Makamba na kwa kadri mchakato wa suala hili unavyokwenda, ni bayana kuwa Serikali safari hii imejipanga kuvifanya vifungashio vya plastiki kuwa historia.

Nasi kama sehemu ya wadau wa maendeleo, tunawiwa kusifu hatua hii na kuiunga mkono hasa kwa kuzingatia kuwa suala la kuachana na matumizi ya plastiki limekuwa likizungumzwa kwa miaka nenda rudi pasipo kufikia mwisho wake.

Kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu Serikali imekuwa ikipambana kuzuia plastiki kwa kuweka mikakati mbalimbali kama ongezeko la kodi kwa zaidi ya asilimia 100, lakini mikakati yote hiyo ilinoa, huku uzalishaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki vikizidi kutamalaki.

Kila mwananchi anapaswa sasa kuunga mkono jitihada hii ya Serikali kwa kuwa kinachofanyika siyo kwa maslahi ya mamlaka husika za kiserikali tu, bali ni kwa faida ya kila Mtanzania na nchi kwa jumla.

Ulinzi na usalama wa mazingira yetu havina budi kuwa wajibu wa kila mwananchi. Na kwa kuwa vifugashio vya plastiki vimekuwa moja ya vyanzo vikubwa vya uharibifu wa mazingira, hatuna budi kuunga mkono vita hii ya Serikali dhidi ya uzalishaji na matumizi yake.

Tunatambua wapo watakaoathirika na mchakato huu, lakini ulinzi wa mazingira yetu ni suala muhimu na kama Watanzania hatuna budi kulipigania kwa kila namna inayowezekana.

Kwa mujibu wa taarifa za Serikali, mifuko ya plastiki pekee licha ya kuwa na uwezo wa kukaa pasipo kuharibika kwa zaidi ya miaka 50, ndio inayochangia kati ya asilimia 80 hadi 90 ya taka zinazoharibu mazingira baharini.

Hiki ni kiwango kikubwa cha uharibifu wa mazingira na ndio maana baadhi ya watafiti wanasema kama hali hiyo itaachwa kubakia ilivyo, upo uwezekano ifikapo mwaka 2050 taka za baharini zitakuwa nyingi kuliko samaki.

Tunapowasihi wananchi kuiunga mkono Serikali katika kampeni hii, hatuna budi kuitanabahisha Serikali kuwa moto iliouwasha unawachoma wengi na wanaweza kufanya kila wawezalo kutaka kuuzima.

Serikali isipokuwa makini inaweza kujikuta inamezwa na ushawishi watu wenye masilahi kwa hoja mbalimbali kama vile kupewa muda wa kujiandaa na nyinginezo ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitumika kudhoofisha kampeni hii.

Tusipokuwa na dhamira madhubuti, mipango na mikakati, tuna wasiwasi kampeni hii inaweza kuwa kama upepo uvumao na kupita, huku tukiacha mazingira ya nchi yetu yakiendelea kuharibika.

Tanzania ni nchi yetu, hakuna pa kukimbilia kama tutaruhusu matumizi ya vifungashio hivi ambavyo siyo tu ni hatari kwa usalama wa mazingira, lakini pia vinasababisha maradhi yakiwamo ya saratani.

Sote tunapaswa kuiunga mkono Ofisi ya Makamu wa Rais katika kampeni hii na kila mmoja hana budi kujiona kuwa ni sehemu ya harakati hizi za kutunza mazingira yetu ambayo wengi duniani wanayatamani.

Share.

About Author

Leave A Reply