Thursday, August 22

Manara wa Simba aibua gumzo bungeni

0


By Habel Chidawali,Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM) Cosato Chumi ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kujifunza kwa msemaji wa timu ya Simba, Haji Manara, kuhusu uhamasishaji anaoufanya kwa timu yake.

Chumi amemtaja Manara leo bungeni Alhamisi Mei 23, 2019 alipochangia hotuba ya wizara hiyo bungeni.

Amesema kama wizara hiyo itachukua mbinu ya mhamasishaji huyo inaweza kuwa imefanya vizuri na kujaza watalii nchini.

“Manara alihamasisha wakati Simba ikicheza na Uganda na tukajaza Uwanja wa Taifa, huyu ni mbunifu wa uhamasishaji katika kila eneo hivyo wizara ikiwa sawa na huyo inaweza kujaza watalii wengi,” amesema Chumi.

Mbali na Manara lakini amewataja Thobias Kifaru wa timu ya Mtibwa na Masau Bwire ambaye ni msemaji wa timu ya Ruvu Shooting.

Kauli ya Chumi kuhusu Simba iliibua kelele za shangwe bungeni baada ya mwenyekiti wa bunge Mussa Zungu kutaka arudie kuitaja timu hiyo.

Kwa mujibu wa Chumi, kama Manara peke yake anaweza kujaza Uwanja wa Taifa, Serikali haitashindwa kujaza watalii nchini Tanzania.

Akizungumza kuhusu misitu na mali zake, amemtaka waziri kuruhusu usafirishaji wa mbao nyakati za usiku ili biashara hiyo isipate vikwazo kufika maeneo husika.

Share.

About Author

Leave A Reply