Sunday, August 18

Manara apagawisha mashabiki soka Pangani

0


By Burhani Yakub

Pangani. Afisa Habari wa Simba SC, Haji Manara alikuwa kivutio kwa mashabiki wa soka waliojitokeza katika sherehe za uzinduzi wa Ligi daraja la nne ngazi ya Wilaya ya Pangani (Awesso Cup) zilizofanyika leo kwenye Uwanja wa Nkumba mjini hapa.

Manara alikuwa miongoni mwa wageni maarufu waliotoka mikoa mbalimbali nchini walioalikwa na Mbunge wa Jimbo la Pangani na Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Awesso kuhudhuria sherehe hizo.

Uwanja ulilipuka kwa mayowe baada ya Mshereheshaji wa sherehe hizo, Bakari kutangaza kuwa Manara amewasili uwanjani hapo kwa kuchelewa na baadaye Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah alimwita jukwaani kuwasalimia mashabiki.

Akizungumza wakati akiwasalimia mashabiki, Manara alisema amekuja Pangani kwa ajili ya kumpa sapoti Mbunge Awesso ambaye ni rafiki yake.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya pamoja na Bongo Movie wanaounda kundi la uzalendo kwanza.

Katibu wa chama cha soka Wilaya ya Pangani, (PDFA), Mussa Lyimo alisema jumla ya timu 14 zinatarajiwa kuchuana vikali katika ligi daraja la nne Wilaya ya Pangani iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.

Alisema ligi hiyo itachezwa katika viwanja vya Nkumba mjini Pangani na Kijiji cha Sakura ambapo inatarajiwa kumalizika Mei 27 mwaka huu ambapo timu zitakazoshiriki ni Black Burn Rangers, Masaika FC, Bama Rangers, Black Mamba, APL Kigombe, Mkwajuni FC, Amboni Plantation Mwera na Mnarani FC.

Timu nyingine ni Black Boys, Small Tigers, APL Sakura, Kambona United, Mapo FC pamoja na 2020 FC.

Share.

About Author

Leave A Reply