Thursday, July 18

Mambo matano yanayombakiza Kotei Simba

0


By Charles Abel

Dar es Salaam. Harakati za klabu mbalimbali za soka nchini kuimarisha vikosi vyao katika kipindi hiki cha dirisha kubwa la usajili, zinaendelea kwa kasi kama sehemu ya kujiandaa na msimu ujao wa 2019/2020.

Ni katika kipindi hiki ambapo klabu zinapunguza wachezaji ambao wameonekana kushindwa kuwa na ufanisi katika msimu uliopita na kusajili wapya lakini pia kuongeza mikataba ya nyota ambao walionekana kutoa mchango mkubwa kwenye vikosi vyao ili waendelee kuzitumikia.

Mabingwa wa Ligi Kuu 2018/2019, Simba ni miongoni mwa timu ambazo tayari zimeshaanza harakati za usajili na yenyewe kwa kuanzia, kipaumbele chake cha kwanza ni kusainisha mikataba mipya kwa baadhi ya wachezaji ambao walionyesha kiwango kizuri ili wanedelee kuitumikia msimu ujao.

Inasemekana tayari imeshaongeza mikataba ya Jonas Mkude, John Bocco, Aishi Manula na Erasto Nyoni huku ikiwa mbioni kuongeza ila ye Shomary Kapombe na Haruna Niyonzima.

Hata hivyo katika hali ya kushangaza inatajwa kuwa Simba bado haijaanza mazungumzo na kiungo raia wa Ghana, James Kotei kwa ajili ya kumpatia mkataba mpya baada ya ule wa awali kumalizika na kwa sasa kiungo huyo ni mchezaji huru anayeweza kujiunga na timu yoyote ile.

Sababu kubwa inayodaiwa kuwafanya Simba wachelewe kumalizana na Kotei ni ile inayotolewa kuwa kocha Patrick Aussems amependekeza kwamba atafutwe kiungo mwingine mwenye ubora na uwezo wa hali ya juu kuliko Kotei ili asajiliwe na Mghana huyo aonyeshwe mlango wa kutokea.

Inawezekana ikawa ni kweli ripoti ya benchi la ufundi imeptoa mapendekezo ya kumuacha Kotei au labda klabu hiyo imemchoka kiungo huyo lakini katika hali halisi, bado kiungo huyo anahitajika ndani ya Simba na zifuatazo ni sababu kadhaa za hilo.

Ingawa aliwahi kupewa adhabu ya kufungiwa mechi kadhaa za Ligi Kuu baada ya kumpiga ngumi Gadiel Michael wa Yanga, Kotei ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa na nidhamu kubwa nje na ndani ya uwanja.

Hajawahi kuwa na skendo na kashfa za nje ya uwanja na ni mchezaji ambaye amekuwa akitimiza vyema majukumu yake kwa timu kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi na kulidhihirisha hilo, aliwahi kuomba radhi haraka baada ya tukio la kumpiga ngumi, Gadiel jambo ambalo hakuwahi kulifanya kabla.

Ni aina ya mchezaji ambaye amekuwa haendekezi starehe na anasa jambo ambalo limemfanya aweze kulinda kipaji chake tangu alipotua nchini mwishoni mwa mwaka 2016

Ni mchezaji mwenye mapafu ya mbwa na anayepambana ndani ya uwanja kwa kila hali kuhakikisha Simba inapata matokeo na amekuwa akiliinda vyema safu ya ulinzi ya timu hiyo kwa kuifanya iwe salama jambo ambalo limeifanya Simba iwe moja ya timu ngumu kufungika katika mashindano mbalimbali hasa yale ya  ndani.

Unapokwenda kushiriki mashindano ya kimataifa kama Ligi ya Mabingwa Afrika, unapaswa kuwa na aina ya wachezaji ambao wanaweza kumpa machaguo tofauti ya kiufundi kocha mkuu pale inapotokea analazimika kufanya hivyo. Mbali na kucheza kama kiungo mkabaji, Kotei anaweza kucheza vyema kama beki wa kati namba nne au namba tano, lakini pia anaweza kucheza kwa ufasaha katika nafasi ya beki wa kulia.

Kumuacha Kotei kwa kipindi hiki kunaweza kupelekea Simba icheze kamali mbaya kama ile iliyocheza baada ya kumaliza msimu wa 2013/2014 ilipoamua kumtema aliyekuwa mfungaji bora wa msimu huo, Amissi Tambwe na kumsajili Dan Sserunkuma aliyekuwa akiichezea Gor Mahia ya Kenya.

Katika kile kinachoonekana ni malipo ya dhambi hiyo ya kumtema Tambwe aliyewaweka mgongoni kwenye msimu mmoja nyuma yake, Sserunkuma alichemsha na kushindwa kuipa kile ambacho ilikihitaji ambacho ni kuwafungia mabao ya kutosha na badala yake akageuka mzigo huku Tambwe akitimkia Yanga ambako aligeuka shujaa na kufanikiwa kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu mara mbili. 

Ni rahisi kutumia kiasi kidogo cha fedha kumpa Kotei ili aongeze mkataba mpya kuliko usajili mpya ambao utailazimisha Simba kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumnasa mchezaji ambaye haina uhakika kama ataweza kuwapa kile wanachokihitaji au la.  


Share.

About Author

Leave A Reply