Friday, August 23

Makonda azungumzia kauli ya wanaojifanya kutetea wanyonge

0


By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema Serikali ya awamu ya tano imekuja kwa ajili ya kuwainua wanyonge wasiokuwa na sauti kupata haki.

Aliyasema hayo jana wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya barabara, elimu, maji na afya katika halmashauri ya Ilala.

“Niliona kuna kauli kuwa kuna watu wanatumia wanyonge kujinufaisha, wanaweza wakawepo, lakini sasa wanyonge wamepata nafasi ya kuitumia Serikali ya awamu ya tano, watu waliokuwa wamesahaulika, wamekandamizwa haki zao  sasa wanazipata kwa wakati,” amesema.

 Makonda amesema kwa uelewa wake awamu hii ndiyo wanyonge wanatamba mtaani hata wakienda kituo cha polisi ama mahakamani wanasikilizwa na wanapata haki.

“Awamu ya tano imekuja kuwainua Watanzania wasiokuwa na sauti,  asiyekuwa na pesa ya kutoa rushwa Rais John Magufuli anasimama kwa ajili yake, imefika hatua sasa dawa zimeongezewa bajeti hadi kufikia Sh270  bilioni, nani kama Magufuli,” amesema.

Kauli hiyo ya Makonda imekuja siku chache baada ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani (KKKTDayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza kuwataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kuwa makini na watu wanaojifanya kutetea wanyonge kwa lengo la kujinufaisha kisiasa, kiuchumi na kiitikadi.

Askofu Bagonza alisema hayo Aprili 19 kwenye ibada ya Ijumaa Kukuu iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Lukajambe wilayani Karagwe mkoani Kagera.
“Niweke angalizo. Unyonge wetu, maradhi yetu, umaskini wetu si mtaji wa wasaka tonge. Bwana Yesu hakunufaika na mateso yale, tulionufaika ni sisi.”
“Kwa hiyo wanaojitoa kutetea wanyonge wawe makini kutoutumia unyonge wetu kujinufaisha kiuchumi, kisiasa, kiitikadi na hata kiimani,” alisema Askofu Bagonza.

Akiwa katika ziara hiyo, Makonda pia aliagiza wazabuni  wanaoshinda zabuni za miradi ya maendeleo katika mkoa huo wanunue malighafi hapa nchini ikiwamo nondo na simenti

Alisema  katika  kipindi cha miaka miwili ndani ya  uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, mkoa wa Dar es Salaam umepokea zaidi ya Sh 2 trilioni na kuwataka wataamu  kuweka mkakati  wa wazawa kupata kazi kwenye kila mradi na kwa wale walioshinda zabuni wanunue malighafi hapa nchini.

  “Hii lazima ifanyike ili uchumi wetu ukue, tusikubali na siyo dhambi anayeshinda tenda aambiwe malighafi anunue hapa, sisi tuna shirika la viwango vya ubora (TBS) iwapo ataona anahitaji ubora wa kitu fulani aseme kitaboreshwa kwa namna anavyohitaji.”

“Msikubali mtu kuagiza bidhaa ambazo hata hapa nchini zipo wakati hawajui ubora wake umekaguliwa na nani halafu baadaye wanaanza kuhangaika kutafuta msamaha wa kodi na mradi unachelewa, wahakikishe wananunua hapa nchini kwa  kuwa kadiri  malighafi hizo zikianza kutumika viwanda vitapanuka na  ajira zitakuwa,” amesema. 

Akiwa katika eneo la ujenzi wa soko la Kisutu, Makonda aliwataka wakandarasi wanaojenga soko hilo kulikabidhi kabla ya wakati wa uchaguzi mkuu mwakani haujafika.

Kwa upande wake, injinia Taher Mjafferji  alieleza  kuwa soko hilo litajengwa ndani ya miezi 18 na kwamba  wanatarajia kumaliza ujenzi huo  mwishoni mwa Desemba mwakani.

Mbali na mradi huo, Makonda  ametembelea ujenzi wa barabara ya Mbarouk katika kata ya Gerezani Kariakoo, barabara ya Kampala Gongolamboto,  ujenzi wa barabara ya Kwa Gude Kiwalani na ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ilala inayojengwa Kivule.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya Kivule, Makonda alisema  awali alikuwapo mkandarasi aliyekuwa akiijenga lakini kukatokea changamoto akasimama hivyo sasa amepatikana mkandarasi mwingine ambapo fedha zipo na anatarajiwa kuanza ujenzi huo mwezi Julai mwaka huu.

Makonda aliagiza hospitali ya wilaya ya Ilala inayojengwa Kivule itakapokabidhiwa Juni 30 mwaka huu na barabara hiyo iwe imekamilika.

Share.

About Author

Leave A Reply