Sunday, August 18

Makipa hawa wamecheza mechi kibao bila nyavu zao kuguswa

0


London, England. Kuwa golikipa bila ya shaka ni kazi ngumu zaidi duniani. Ni rahisi kupewa lawama na kosa moja tu linaweza kuwasahaulisha watu mazuri yako yote.

Ni kazi ngumu pia kuwa kipa bora kwenye michuano ya aina yoyote ile kama ya Ligi Kuu England iliyojaa ushindani mkubwa.

Hakuna ubishi, Ligi Kuu England ni moja yenye ushindani mkubwa sana duniani, lakini kuna makipa hao wametamba kwenye ligi hiyo ya kibabe wakicheza mechi kibao bila ya kuruhusu mipira kugusa nyavu zao.

Hii hapa orodha ya makipa waliofikisha mechi 20 na kuondelea ndani ya msimu mmoja wa Ligi Kuu England wakicheza bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa. Data hizi ni kwa mujibu wa Sky Sports.

5. Alisson (mechi 20, msimu 2018/19)

Liverpool imekuwa ikifurahia msimu wao msimu kabisa huko kwenye Ligi Kuu England na kufukuzia ubingwa wakichuana jino kwa jino na Manchester City. Kwa msimu huu, kikosi kizima cha kocha Jurgen Klopp kimeonekana kuwa kwenye ubora mkubwa akiwamo kipa wao, Alisson Becker, ambaye ni matata kwelikweli golini, akiwa ameshacheza mechi 20 bila ya wavu wake kuguswa.

Alisson alinaswa mwaka jana kwa pesa ndefu akitokea AS Roma na hakika malipo ya pesa yao yamekwenda vyema kutokana na kipa huyo hadi sasa kuruhusu wavu wake kuguswa mara 20 tu katika mechi walizocheza kwenye Ligi Kuu England.

4. Pepe Reina (mechi 20, msimu 2005/06)

Kwenye rekodi zake, kipa Pepe Reina alikuwa moto kwelikweli, akiwa rekodi ya kutoruhusu wavu wake kuguswa kwa zaidi ya mechi 20 katika misimu miwili tofauti. Alifanya hivyo kwenye msimu wa 2005/06 na kurudia 2008/09, ambapo misimu yote alicheza mechi 20 bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa. Bahati mbaya katika misimu yote hiyo Reina alishindwa kuipa Liverpool ubingwa wa ligi na kuishia tu kubeba mataji mengine. Katika msimu wa 2008/09, Reina aliruhusu wavu wake kuguswa mara 27 tu, huku mechi 20 katika msimu huo alizotoa kapa timu za wapinzani kugusa wavu wake.

3. Peter Schmeichel (mechi 20, msimu 1994/95)

Gwiji wa Manchester United, kipa Peter Schmeichel anakumbukwa kwa mambo mengi kwenye kikosi hicho, lakini kubwa ni vile alivyokuwa akiwahamasisha wachezaji wenzake wacheze kwenye kiwango cha juu siku zote.

Katika msimu wa 1994/95 kwenye Ligi Kuu England, Schmeichel, alikuwa moto kwelikweli golini na kuisaidia Man United kuwa vizuri kwenye mbio za ubingwa. Katika msimu huo, kipa huyo alicheza mechi 20 bila ya kuruhusu mpira kugusa kwenye wavu wake, katika msimu uliochezwa mechi 42 ambapo Blackburn Rovers waliibwaga Man United kwa pointi moja tu katika ubingwa.

2. Edwin van der Sar (mechi 21, msimu 2008/09)

Katika msimu wa 2008/09, Manchester United iliwapa mapigo mawili Liverpool. Si tu kwamba waliwatesa wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa bali kipa wao pia, Van der Sar alimbwaga Pepe Reina wa Liverpool kwenye tuzo ya kipa bora wa msimu.

Januari 27 katika msimu huo, Van der Sar aliweka rekodi ya kucheza mechi nyingi mfululizo bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa kwenye Ligi Kuu England wakati alipocheza mechi 11 na dakika 1,032 bila ya mpira kutinga kwenye wavu wake. Alifungwa mabao 24 tu katika msimu huo, huku mechi 21 akicheza bila ya wavu wake kuguswa.

1. Petr Cech (mechi 24, msimu 2004/05)

Petr Cech bila shaka ni moja ya makipa bora kabisa waliowahi kutokea kwenye Ligi Kuu England na hakika kwenye msimu wa 2004/05 alikuwa kwenye kikosi bora kabisa kwenye ligi hiyo.

Machi 2005, kipa huyo kipindi hicho alipokuwa Chelsea aliweka rekodi mpya kwenye Ligi Kuu England kwa kucheza dakika 1,025 bila kuruhusu mpira kugusa kwenye wavu wake kabla ya kuja kuruhusu bao katika mechi dhidi ya Norwich City. Rekodi hiyo ilikuja kuvunjwa na Edwin van der Sar. Katika msimu huo, Cech alicheza mechi 24 bila ya kuruhusu bao katika mechi 35 alizocheza.

Share.

About Author

Leave A Reply