Saturday, August 17

Majaji wa Rufani kujiwekea malengo ya mwaka 2019

0


By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Majaji wa Mahakama ya Rufani wamekutana katika mkutano wao wa mwaka kwa lengo la kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kutoa haki kwa mwaka uliopita wa 2018 na kujiwekea malengo ya utendaji bora kwa mwaka huu wa 2019.

Katika mkutano huo wa siku mbili uliofunguliwa leo Jumanne, April 23, 2019 na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, majaji hao watapata mafunzo maalum yaliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), kilichoko Lushoto mkoani Tanga.

Pamoja na mambo mengine majaji hao watajifunza majukumu ya wenyeviti wa majopo ya majaji wakati wa usikilizaji kesi na wajibu au mchango wa majaji wengine katika jopo husika.

Mafunzo hayo yatawezeshwa na majaji wastaafu watatu wa Mahakama ya Rufani ambao watatoa uzoefu wao.

Majaji hao wastaafu wa Mahakama  ya Rufani ambao ni wawezeshaji ni pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, January Msoffe, Jaji wa Mahakama ya Juu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sauda Mjasiri na John Mrosso.

Akifungua mkutano huo Jaji Mkuu, amesema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Mahakama ya Rufani ndio mahakama  ya juu na yenye uamuzi wa mwisho katika utoaji haki nchini.

Amesema kuwa mikutano ya mafunzo na tathmini ni muhimu katika kuwasaidia majaji kuwapa uwezo wa mwisho katika kutoa haki kwa kuzingatia sheria na misingi ya haki na hivyo kuendelea kujenga imani ya utumishi kwao wenyewe majaji na katika mfumo mzima wa utoaji haki.

“Nafasi yetu katika jukumu letu la utoaji haki inatupa wajibu mkubwa katika mambo mengi,” amesema Jaji Mkuu katika  hotuba yake ya ufunguzi na kuongeza: “Mamlaka yangu hayatokani tu na kutoa haki kwa mujibu wa sheria kwa sababu kama mahakama ya mwisho vilevile tuna wajibu wa kutoa uamuzi katika masuala yote ya haki hata yale ambayo hayajatungiwa sheria yoyote.”

Jaji Mkuu amewataka majaji hao kujadiliana kwa kina ili kuibua tamaduni ambazo ni nzuri watakazozitumia katika utoaji wa haki.

Share.

About Author

Leave A Reply