Saturday, August 24

Maisha ya Ellen Sirleaf nyuma ya Tuzo ya Mo-Ibrahim

0


Januari 22, mwaka huu, Ellen Johnson Sirleaf alikabidhi uongozi wa Liberia kwa mrithi wake, George Weah baada ya kuongoza kwa miaka 12. Ndani ya mwezi mmoja tangu aondoke madarakani, Sirleaf ametunukiwa tuzo ya uongozi uliotukuka ya Mo Ibrahim akiwa wa tano Afrika.

Hii ni tuzo ngumu kwa viongozi wa Afrika. Tuzo ambayo imekuwa na matundu mengi kwa sababu ya kupitisha miaka bila kupata washindi.

Kamati ya tuzo ya Mo Ibrahim, imeona Sirleaf anastahili kutunukiwa tuzo hiyo kwa sababu ya namna alivyoituliza nchi na kuunganisha watu wa Liberia kuwa jamii moja katika mazingira magumu na kurejesha utu, haki na demokrasia baada ya miongo minne ya machafuko.

Sirleaf ni kielelezo cha kila mwenye kuonekana hawezi kuwa anaweza. Akiwa na umri wa miaka 17, baada ya kuona hali ngumu nyumbani kwao, Sirleaf aliona bora aolewe. Alichagua kuolewa na kuacha kwenda chuo kwa sababu ya kutafuta urahisi wa maisha.

Aliolewa na mtaalamu wa kilimo, James Sirleaf na aliishi katika ndoa iliyojaa manyanyaso na alizaa mfululizo.

Unyonge hadi ushujaa

Juhudi za Sirleaf kubadili unyonge kuwa ushujaa zilianza mwaka 1961. Mwaka huo mume wa Sirleaf, alipewa udhamini wa masomo Serikali ya Liberia, kwenda Marekani kusomea shahada ya umahiri wa kilimo. Sirleaf aliona hiyo pia ni fursa kwake.

Ikabidi naye aombe udhamini serikalini kwenda Marekani. Awali alitegemea angepata kwa urahisi kwa sababu baba yake alikuwa seneta na alikuwa akifahamika mno ndani ya ofisi za Serikali lakini matokeo yalikuwa tofauti.

Kwa vile Sirleaf aliona hiyo ndiyo ilikuwa fursa pekee ilibidi apande na kushuka kubembeleza serikalini, hatimaye alifanikiwa kupata udhamini wa kwenda kusoma Marekani, changamoto kubwa ikawa watoto wake.

Kusafiri nao kwenda Marekani kwenye masomo ilikuwa ni jambo gumu. Kwanza kiuchumi, pili mateso, maana wao wangekuwa wanabanwa na masomo, nani angewatazama?

Kuwaacha Monrovia ulikuwa ni mtihani mwingine kwa sababu walikuwa wadogo na wa mwisho alikuwa hajatimiza hata mwaka mmoja, wa tatu akimzidi kidogo. Jumla watoto wote wanne walikuwa chini ya umri wa miaka minne.

Baada ya kutafakari kwa muda mrefu, uamuzi ukawa ni kuwaacha watoto Liberia. Waligawanywa, wawili walilelewa na mama yake Sirleaf, wengine walibaki mikononi mwa mama yake mumewe, maarufu kama Doc.

Walisafiri vizuri kwenda Marekani, Sirleaf anasema: “Nilipokuwa nawaaga watoto wangu niliumia sana. Upendo wangu kwa watoto wangu ni mkubwa lakini sikuwa na jinsi, niliwaacha.”

Wakati mumewe anasoma shahada ya uzamili katika kilimo, yeye alianza shahada shirikishi ya uhasibu.

Mume hakutaka mfanikio yake

Kama ilivyo kwa wanaume wengi kutaka wake zao kuwa chini, ndivyo ilivyokuwa kwa Doc. Basi, ilikuwa kawaida kwa Sirleaf kupokea mkong’oto na kutishiwa bastola.

Shida kubwa ambayo ilianza kuwagombanisha nchini Marekani, ni pale Sirleaf alipoamua kufanya vibarua vya hapa na pale ili aweze kusaidiana na mume wake kujikimu kiuchumi.

Miongoni mwa kazi ambazo Sirleaf alizifanya ni ufagiaji. Doc hakupenda mkewe afanye kazi hiyo, aliona kama anamdhalilisha. Sirleaf alisimamia ukweli kuwa walihitaji fedha. Aibu aliweka pembeni.

Kwa uamuzi huo, Doc alishamvamia Sirleaf eneo lake la kazi, akamnyang’anya ufagio na kuutupa, akampiga vibao mbele za watu kisha akamshinikiza atangulie mbele kurudi nyumbani.

Doc alikuwa mlevi, asiyemjali mkewe, tatizo dogo lilimuongoza kumpiga na kumtishia bastola. Na vile alikuwa mwanajeshi, basi mafunzo yote ya kijeshi alitamani kuyamalizia kwa Sirleaf.

Sirleaf alikuwa anafanya kazi ya ufagiaji kwenye duka la Rennebohm Drug Store na kwa kitendo cha Doc kumvamia na kumfanyia fujo eneo la kazi, ilikuwa kidogo aachishwe kibarua hicho.

“Kazi ilitupa fedha ambazo tulizihitaji sana, nilikwenda kwa bosi wangu, akaniambia Ellen wewe ni mchapakazi mzuri, sasa kama kweli hii kazi unaipenda basi mwambie mumeo asije tena.

“Nilimwambia Doc asije tena pale kazini na kweli hakuja ila migogoro ikawa inahama kutoka hatua mbaya hadi kuwa mbaya zaidi. Doc alitaka akiwa nyumbani anione, nami nilikuwa napambana kutafuta fedha,” anasema Sirleaf.

Ndani ya kitabu chake kinachoitwa This Child Will Be Great (Huyu Mtoto Atakuwa Mtu Mkubwa), Sirleaf anaeleza kuwa kutokana na juhudi zake kazini, alipandishwa daraja kutoka mfagiaji hadi kuwa ofisa malipo.

Kwa kupandishwa kwake cheo na fedha ziliongezeka lakini Doc alinuna. Alitamani kumuona akiwa mama wa nyumbani tu. Sirleaf anasema: “Jinsi nilivyofanikiwa ndivyo alivyonikasirikia, na ndivyo ugomvi ndani ya nyumba ulivyopamba moto.”

Doc alikuwa wa kwanza kumaliza shahada yake ya uzamili, akarejea Monrovia na kumwacha Sirleaf akiendelea na masomo ambaye naye baada ya kuhitimu, alirudi Liberia na kuajiriwa serikalini kama ofisa wa hazina.

“Nilifanya kazi kwa bidii sana. Kila nilivyojituma ndivyo nilipanda ngazi kikazi lakini ndivyo na mume wangu alivyopoteza furaha. Tukaendelea kuishi maisha ya migogoro nchini Liberia, ugomvi ulikuwa mkubwa na mume wangu alinipiga sana.

“Kuna siku nilimkuta nyumbani akiwa ameshika bastola, akaniambia siku hiyo ndiyo kifo changu, akanielekezea kuwa anataka kuniua. Mtoto wangu wa kwanza ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka nane, alilishuhudia lile tukio, yeye ndiye aliniokoa, alimvamia baba yake na kumwambia asinifanye chochote,” anasema Sirleaf.

Anaongeza: “Doc alichanganyikiwa kwani hakutegemea kama mtoto angeona. Clave aliniambia kumng’ang’ania Doc ni sawa na kulazimisha kifo. Nilimwelewa na tulikubaliana kufungua mahakamani madai ya talaka.

Sirleaf aliamini kuwa kwa vile Doc alikuwa na wanawake wengine, asingepinga kumpa talaka lakini hakuhudhuria mahakamani na alikuwa akimfuata kwenye nyumba aliyohamia kumfanyia fujo. Pona ya Sirleaf ilikuwa pale Doc alipooa mwanamke mwingine kisha akaenda Marekani ndipo akajikita kuyatafuta maendeleo ya kimaisha ambayo yamemfikisha alipo leo.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.