Sunday, August 18

Mahrez amtolea uvivu Guardiola

0


London, England. Mchezaji aliyetia fora kwa usajili Manchester City, Riyad Mahrez amesema amechoka kusugua benchi na yuko tayari kuondoka katika kikosi hicho.

Licha ya kusajiliwa kwa bei mbaya Pauni60 milioni akiwa ndiye mchezaji aliyetua kwa fedha nyingi Man City, lakini Riyard amekosa namba katika kikosi cha kwanza.

Kocha wa Man City Pep Guardiola alivutiwa na kipaji chake akiwa Leicester City na hakusita kuvunja benki kumsajili majira ya kiangazi msimu uliopita.

Pamoja na uhodari wake ulioipa Leicester City ubingwa wa England, lakini baada ya kutua Man City hali imekuwa mbaya.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Algeria ameingia akitokea benchi katika mechi tatu zilizopita hatua iliyoibua maswali kama atabaki Etihad msimu wa majira ya kiangazi.

Mahrez mwenye miaka 28 anaweza kuchukua uamuzi mgumu wa kuondoka majira ya kiangazi kusaka klabu ambayo itampa nafasi ya kucheza.

Kiungo huyo wa pembeni amefunga mabao sita na kutoa pasi za mwisho mara ya tatu katika mechi 26 alizocheza Man City tangu alipojiunga na klabu hiyo.

Guardiola alimpanga nyota huyo badala ya Leroy Sane katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hakuonyesha kiwango bora.

Kocha huyo aliwahi kutamka kuwa Mahrez ni mchezaji anayefanya vyema katika mazoezi na alimuomba radhi kwa kitendo chake cha kumuweka benchi.

Share.

About Author

Leave A Reply