Friday, April 19

Maguli: Mnasemaje nyie, Okwi amekwisha?

0


By Olipa Assa

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa KMC, Elias Maguli amesema licha ya Emmanuel Okwi kuonekana kama anapotezwa na Mnyarwanda Meddie Kagere kwenye macho ya mashabiki, ukweli ni kwamba jamaa bado ana vitu vingi adimu miguuni mwake.

Maguli amesema, kila anapomfatilia mshambuliaji huyo wa Simba uwanjani, anabaini ni hatari kwa mbinu na kudai ni kati ya wachezaji wachache tishio ndani na nje ya nchi.

“Naangalia aina ya mabao anayofunga mfano lile alilotupia kwa JS Saoura,  alitumia akili nyingi kwani kama angekuwa mshambuliaji mwenye maamuzi sahihi asingeweza kufunga. Alifanya maamuzi ya haraka akiwa katikati ya mabeki,” alisema Maguli.

Alisema tangu aanze kumfahamu, Okwi amejifunza vitu vingi vinavyomfanya aendelee kuwa yule yule na kudai ingawa kwa sasa Kagere ndiye anaonekana kukubalika zaidi kwa mashabiki lakini ufundi wa mchezaji huyo hauwezi kufutika.

“Okwi amefanikiwa sana kwenye nidhamu ya kazi yake lakini pia hana mambo mengi uwanjani zaidi ya kufanya kazi yake kwa bidii. Kwa mchezaji  anayecheza Simba na Yanga akifanikiwa kucheza na hisia za mashabiki anaweza kufika mbali. Sifa za Okwi anapewa na mashabiki lakini si kama yeye anazitaka,”alieleza Maguli.

Naye nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema Okwi anajua nini maana ya tafsiri ya soka, akisisitiza kuwa bado ana madini yenye mvuto mguuni mwake.

“Bado Okwi ana nafasi yake kubwa katika soka la Tanzania, anajua kutengeza nafasi, hana papara, anatumia akili nyingi, anakaa na mipira na imani yangu bado atafanya kitu kwenye ligi hii,” alisema Mogella.

Share.

About Author

Leave A Reply