Friday, July 19

Magufuli apewa ushauri kuteua viongozi THBUB

0


Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umemuandikia barua Rais John Magufuli kumuomba ateue viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ambayo kwa karibu mwaka mmoja haina uongozi.

Aliyekuwa mwenyekiti wa THBUB, Bahame Nyanduga alistaafu Desemba 2017 baada ya kumaliza muda wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu waraka huo kwa Rais, mratibu wa mtandao huo, Onesmo Olengurumwa alisema inasikitisha kuona kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja nchi imekuwa ikiendeshwa bila kuwapo kwa tume halali ya haki.

“Kwa mujibu wa Katiba, Tume inasemekana kuwa kamili au kuwepo kisheria wakati mwenyekiti wake na makamishna wanapokuwepo ofisini,” alisema Olengurumwa.

Alisema hali hiyo imesababisha kuendelea kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na misingi ya utawala kunakofanywa na baadhi ya watumishi wa umma na kwamba hata Rais mwenyewe anakosa mshauri wa masuala kama hayo.

“THRDC inaamini kwamba masuala mengi ya haki za binadamu hayachukuliwi hatua kwasababu Tume haipo kisheria. Tume imeshindwa kuishauri Serikali na mihimili mingine ya umma kuhusu masuala ya utawala na haki ambayo yanaathiri nchi kwa sasa,” alisema.

Kauli hiyo inakuja wakati jumuiya ya kimataifa pamoja na wana harakati nchini wamekuwa wakilalamikia ukiukwaji wa haki za binadamu.

Wakili wa THRDC, Deogratias Bwire alisema hali hiyo imesababisha nchi kukosa wawakilishi kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa inayohusu haki na utawala, kama ule wa Tume ya Afrika ya Haki za binadamu na Watu wa Oktoba 2018.

Makamishna wengine wanaoonekana katika tovuti hiyo waliomaliza muda wao ni pamoja na Rehema Ntimizi, Rajab, Mohamed Hamis na Salma Hassan.

Share.

About Author

Leave A Reply