Tuesday, August 20

Mabao ya Simba gumzo tupu Kanda ya Ziwa

0


By Saddam Sadick

MWANZA. MAAJABU! Ndivyo unaweza kusema kutokana na matokeo ya michezo minne iliyocheza timu ya Simba kwenye Ukanda wa Ziwa ambayo ukiyaangalia unastuka.

Unajua ikoje? Wekundu hawa wameshangaza sana matokeo yao katika michezo ya Kanda ya Ziwa, kwani kila mchezo waliocheza ulimalizika kwa timu kudunguliwa mabao mawili.

Simba ilianzia mjini Bukoba Aprili 20 kuparuana na Kagera Sugar, ambako ilikubali kulala kwa mabao 2-1, kisha kuigeukia Alliance FC na kushinda mabao 2-0.

Kama haitoshi, Simba iliendelea kushangaza pale ilipokutana na KMC na kujikuta ikitoka uwanjani kwa ushindi wa mabao 2-1 na mwisho kumalizia mkoani Mara kwa kuirarua Biashara United mabao 2-0.

Ukiachana na ya Kanda ya Ziwa, Simba ilikuwa ni mchezo wake wa tano mfululizo ikiendeleza maajabu ya matokeo kama hayo baada ya kuichapa Coastal Union mabao 2-1.

Hata hivyo, katika mazungumzo yake Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Ausems alikaririwa akisema wanachohitaji ni pointi tatu licha ya ratiba kuwa ngumu na kwamba wachezaji wanachoka.

Alisema mkakati wao ni kutetea ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo ili kuendelea kuwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na kwamba anafurahi kwa matokeo wanayopata.

“Vijana wanapambana licha ya ratiba kuwa ngumu. Ninachofanya ni kuwapumzisha baadhi ya wachezaji ili kuendana na hali halisi,” alisema Aussems.

Share.

About Author

Leave A Reply