Thursday, August 22

Lugola: Trafiki atakayepiga ‘tochi’ yenye utata kukiona

0


By Lilian Lucas,Mwananchi [email protected]

Morogoro. Askari yeyote wa usalama barabarani atakayepiga picha ya mwendokasi wa gari ataondolewa katika kikosi hicho

Mbali ya kuchukuliwa hatua hiyo iliyotangazwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, askari huyo atalipa faini ya kosa hilo.

Waziri Lugola alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa mara baada ya kumalizika kwa kikao na wadau wa usalama barabarani.

Alisema mbali na kupata malalamiko kutoka kwa wadau hao, pia amekuwa akipata malalamiko kutoka kwa madereva maeneo mbalimbali juu ya vitendo vya uonevu kutoka kwa baadhi ya askari wa kikosi hicho.

Aliwataka askari wanaohusika na upigaji picha za mwendokasi barabarani kuhakikisha picha inayopigwa inaonyesha gari halisi, mwendo na iwe inaonyesha kwa mbele na si vinginevyo.

Alisema kitendo cha askari kupiga picha yenye utata isiyoonyesha chochote ni kujitengenezea njia ya kuomba rushwa hivyo kuanzia sasa, askari hao wahakikishe wanazingatia upigaji picha kwa umakini ili kuondoa utata na malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Napenda kutoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuondoa kero ya tochi. Askari hakikisheni tochi inatumika kupiga kwa usahihi tena gari lipigwe kwa mbele picha ambayo itaonyesha usajili wa gari husika, hiyo itarahisisha dereva kuamini na kuondoa mvutano,” alisema.

“Naridhia kwa picha itakayoonyesha mambo yote bila kuwepo kwa utata, sheria zitumike na dereva atozwe faini bila woga wowote,” alisema.

Waziri huyo aliwataka madereva kuendelea kuheshimu alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizokuwa za lazima, huku akilitaka Jeshi la Polisi kutoa adhabu kwa dereva anayerudia makosa kwa kumnyang’anya leseni

Share.

About Author

Leave A Reply