Tuesday, March 19

Lowasa katikati ya CCM, Chadema

0


Dar es Salaam. Wapinzani nchini wamesema mfululizo wa kauli za viongozi wakuu wa CCM kumsifia waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ni mchezo wa kisiasa wenye lengo la kuwafarakanisha na pia kutaka kuzima fukuto ndani ya chama hicho tawala.

Baadhi ya viongozi wa upinzani, hasa wa Chadema, ambako Lowassa ni mjumbe wa Kamati Kuu, wanasema sasa ni wakati wa waziri huyo mkuu wa zamani kujitokeza hadharani kusafisha hali ya hewa.

Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amekuwa akimmwagia sifa Lowassa, akimuelezea kama kiongozi mzalendo wa kweli, mstaarabu aliye tofauti na viongozi wengine wa upinzani.

Wiki iliyopita wakati akizindua maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais alirudia tena sifa hizo, akisema Lowassa ni mwanasisasa mstaarabu ambaye baada ya kushindwa mbio za urais 2015 alikubali matokeo.

Hivyo, alimtaka Lowassa awashauri watu anaowaongoza watulie, akisema la sivyo wataishia gerezani. Siku hiyo, Lowassa alimpongeza pia Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya.

Julai mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na viongozi wakuu wastaafu Ikulu Dar es Salaam, pia alitoa sifa kama hizo kwa Lowassa akimuita kuwa ni “mtu mwema sana” ambaye hakuwahi kumtukana.

Juzi usiku, sifa hizo zilidakwa na katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliyesema Lowassa hana unafiki kwa sababu aliondoka ndani ya chama hicho baada ya kukosa ridhaa ya kugombea na kwenda chama kingine (Chadema) badala ya kubaki ndani kinafiki na kuwagawa wanachama.

Sifa anazomwagiwa Lowassa na viongozi wakuu wa CCM zimekuwa zikiibua mijadala na wakati mwingine maswali, baadhi wakihisi kuwa chama hicho kinamhofia na wengine wakidhani jina lake linatumika kuwagawa wapinzani ambao wanaonekana kutojua moyo wa mwanasiasa huyo mkongwe umelala wapi.

Lakini, Dk Bashiru alikanusha tuhuma kwamba wana hofu na umaarufu wa Lowassa na wanatumia jina lake kuwagawa wapinzani.

Alisema wapinzani waache uvivu wa kufikiri kwa kudhani kuwa Lowassa anatumika na badala yake wajenge mifumo imara ya vyama vyao kwa sababu CCM imerudisha imani kwa wananchi.

Alisema kinachofanywa sasa na Rais Magufuli ndiyo kinauua upinzani kwa kuwa walizoea kuchukua umaarufu wa rejareja kwa kudandia upungufu wa baadhi ya viongozi waliokiteka chama kwa kujimilikisha mali na kuishi maisha ya anasa na familia zao.

“Wamezoea kudandia wanachama kutoka CCM wanaokuwa na nuru ya chama kama walivyofanya kwa Dk Willibrod Slaa aliyekuwa Katibu wa Chadema, Augustine Mrema wa TLP na Lowassa,” alisema Dk Bashiru.

“Nuru zao huwa hazidumu. Waache kudandia watengeneze viongozi wao wenye majina na ushawishi.”

Alipotafutwa kuzungumzia sifa hizo na hali inavyoendelea ndani ya upinzani, Lowassa hakutaka kutoa maoni yake.

“Nasema hivi dada yangu, siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa,” alisema Lowassa akiendeleza utamaduni wake wa kutoshiriki mijadala inayomuhusu.

Lakini wapinzani walikuwa na maoni tofauti kuhusu sifa hizo kwa kiongozi aliyeweka upinzani mkubwa katika historia ya siasa za ushindani nchini.

“Lowassa bado anaisumbua CCM, ndiyo maana wanamtaja kupoza mhemko wa wana-CCM walio ndani ya chama,” alisema mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alipozungumza na Mwananchi jana.

Alisema sifa wanazommwagia ni kujaribu kuonyesha kuwa Lowassa hana kinyongo na CCM ili kuwavunja nguvu wanaomuamini ndani ya chama hicho.

Lakini katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema anaamini CCM wanamtumia Lowassa kuwafarakanisha.

Alisema wanajua (CCM) Lowassa ana nguvu kubwa akiwa upinzani kama ilivyoonekana kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita na ndiyo maana wanajaribu kumdhoofisha.

Hata hivyo, Dk Mashinji alisema bado wanaendelea kumuamini Lowassa na yumo kwenye mipango yao.

Naye katibu mkuu wa NLD, Tozi Matwanga alisema CCM wana mashaka na hofu dhidi ya nguvu ya Lowassa hivyo wanajaribu kujitetea wakati huu Uchaguzi Mkuu unapokaribia.

“Naona wazi ndani ya CCM hakuko shwari, wanaomuunga mkono Lowassa ni wengi na wana nguvu ndani ya chama ndiyo maana maonyo na makatazo yamekuwa mengi,” alisema.

Naibu katibu mkuu wa Chadema- Zanzibar, Salum Mwalimu alisema ni wakati sasa wa Lowassa kujitokeza na kuweka msimamo hadharani.

Share.

About Author

Leave A Reply