Friday, August 23

Liverpool uso kwa uso Barcelona ya Messi, Ajax kwa Spurs

0


London, England. HABARI ndiyo hiyo. Ule utamu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya umerudi wiki hii, leo Jumanne kitapigwa kipute cha kwanza cha nusu fainali huko London, wakati Tottenham Hotspur itakapoikaribisha Ajax, wakati shughuli pevu zaidi itakuwa kesho Jumatano huko Nou Camp, Liverpool watakapokwenda kumkabili Lionel Messi.

Macho ya wengi yatasubiri kuona kama ngome ya Barcelona itakuwa kwenye mateso makubwa itakapokutana na fowadi ya wakali watatu moto kabisa wa huko Anfield, Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino wakati watakapokwenda kufanya yao huko Nou Camp.

Kwenye mchezo huo, beki anayetajwa kuwa bora zaidi kwa sasa, Virgil van Dijk atakuwa kwenye mtihani mzito wa kumkabili Messi na jeshi lake ambalo litawahushuhudia Luis Suarez na Philippe Coutinho.

Mechi hiyo itawakutanisha Liverpool na wakali wao wa zamani Suarez na Coutinho na hicho ndicho kinachowafanya kuwapo kwa mvuto mkubwa kwenye mechi hiyo ambapo Barcelona wao watakuwa hawana presha yoyote kwa maana tayari wameshajibebea taji la La Liga.

Huko London, Spurs watakuwa na kazi ngumu kuwakabili Ajax ambao hadi kufika hapo nusu fainali imewatupa nje vigogo Real Madrid na Juventus tena kwa kushinda ugenini.

Kikosi cha kocha Mauricio Pochettino kina mastaa kibao waliotoka Ajax, lakini hakuna ubishi wababe hao wa Uholanzi kwa sasa ndiyo wenye wachezaji walio kwenye viwango bora kabisa kiasi cha kuwafanya vigogo kibao kuwapigia hesabu kuwasajili.

Spurs itawakosa Moussa Sissoko, Serge Aurier na Erik Lamela, wakati Ajax wao watakuwa na karibu na mastaa wake wote wakiwamo Matthijs de Ligt, Frenkie de Jong, David Neres na Dusan Tadic.

Nusu fainali hizo za kwanza zitapigwa wiki hii, wakati mechi za marudiano zitakuwa wiki ijayo, ambapo mwenye ushindi mzuri ndiye atakayefika fainali, huku Liverpool wao wakisaka fainali yao ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kufika hatua hiyo na kuchapwa na Real Madrid.

Share.

About Author

Leave A Reply