Tuesday, August 20

LHRC yatua Kigoma kutoa elimu ukatili wa kingono

0


By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimewataka wakazi wa kata ya Mwanga Kusini mkoani Kigoma kwa kushirikiana na Serikali za mitaa kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kuwalinda wanawake wasifanyiwe ukatili wa kingono.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Mei 18, 2019 na mkurugenzi mtnedaji wa LHRC, Anna Henga katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wasaidizi wa sheria na waangalizi wa haki za binadamu Kanda ya magharibi.

Amesema pamoja na kuunda kikosi kazi cha kuwasaka wanaofanya ukatili huo kwa wanawake, wanaofanyiwa vitendo hivyo  nao wanapaswa kutoa taarifa katika vyombo vya usalama.

“Kazi yangu ni kutetea haki za watoto na wanawake na nimefika Kigoma mwenyewe ili niweze kujionea kwa macho maana awali nilikuwa tu nasikia na nimezungumza nao baadhi nimeamini hili jambo lipo, naamini kwa kushirikiana litaisha,” amesema Henga.

Ofisa mratibu wa masuala ya ulinzi na usalama wa LHRC,  Renatha Selemani amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo baada ya kuona kuna hatari nyingi za kiusalama ambazo zinawakabili watetezi wa haki za binadamu.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Happiness Evarist amesema wanakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo jamii kutojua sheria na haki zao, huku akidai kutumia mafunzo hayo kwenda kuelimisha jamii.

Share.

About Author

Leave A Reply