Wednesday, August 21

Kwaheri Ligi Kuu, huu ni wakati kujisahihisha pale mlipojikwaa

0


By Mhariri

PAZIA la Ligi Kuu Bara msimu huu linafungwa rasmi jioni ya leo (kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote kwa vile ligi hiyo haitabiriki) kwa klabu 20 kupepetana kwenye viwanja 10 tofauti vilivyopo jijini Dar es Salaam na mikoani.

Ligi inafikia ukomo baada ya siku 279 za pilikapilika, vitimbi, vioja na maajabu yaliyojiri tangu kipyenga cha msimu kupulizwa rasmi Agosti 22, mwaka jana. Ni ligi iliyokuwa na changamoto nyingi ambazo hata kufikia kwake salama ni jambo la kumshukuru Mungu.

Kukosekana kwa Mdhamini Mkuu, kuwepo kwa ratiba ya ovyo na panga pangua isiyoisha na kusababisha baadhi ya timu kuwa na mechi za viporo vingi na maamuzi yenye utata kutoka kwa baadhi ya waamuzi ni mambo yaliyojitokeza msimu huu.

Ongezeko la timu kutoka 16 hadi 20 ni kati ya mambo yaliyoifanya ligi iwe ndefu na kuzikwaza baadhi ya timu hasa zile zenye uchumi mdogo, mbali na changamoto ya ratiba kubadiliska kila mara kama kinyonga ni jambo jingine lililoziongezea mzigo klabu.

Inawezekana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi (TPLB) kushangilia kuhitimishwa kwa ligi hiyo leo, huku tayari bingwa akiwa ameshapatikana na timu moja ya kushuka daraja nayo ikifahamika mapema, lakini ni lazima wajitathmini. Kuna mahali TFF/TPLB waliteleza kutokana na mkanganyiko wa ratiba na hata baadhi ya maamuzi ambayo wamekuwa wakiyafanya kwa baadhi ya mechi.

Kwa mfano baada ya kutolewa kwa ratiba ya msimu huu mapema katikati ya mwaka jana, TPLB ilibadilisha ratiba ikiwamo mechi ya Mtibwa Sugar na Yanga ilipaswa kuchezwa Morogoro kurejeshwa Dar na Yanga kuwa mwenyeji dhidi ya Wakata Miwa.

Kuna mechi ya Yanga na JKT Tanzania ilivyoyumbishwa mara Dara, Tanga na kisha Dar kabla ya kubadilishwa tena muda wa kufanyika kwake kutoka saa 8 mchana, 1 usiku hadi saa 10 jioni ni baadhi ya dosari ambazo lazima wasimamizi wa ligi ajitathmini.

Kadhalika kuwepo kwa mechi za ligi zinazoendana na uwepo wa mechi kubwa za kimataifa ni kitu kilichochangia baadhi ya mechi kukosa mashabiki kama ile ya Tanzania Prisons dhidi ya Biashara United ulioingiza kiasi cha Sh 9,000 tu kwa kuingiza mashabiki watatu waliolipa kiingilio. Hii ilikuwa kali ya mwaka katika msimu huu.

Kuna mambo mengi yaliyojiri ikiwamo wafungaji wa hat trick kushindwa kupewa mipira ya mechi waliyofunga mabao matatu na badala yake kutakiwa kuifuata jijini Dar nacho ni kichekesho kama ilivyo kwa kukosekana kwa mipira ya kutosha kwenye mechi za mikoani na kwingine kiasi cha kuifanya Simba kila inapoenda kucheza kutumia mipira yake.

Hatuyasemi haya kama kutaka kumlaumu mtu, ila kusudio letu ni kutaka TFF/TPLB na wadau wa soka kwa ujumla kufanya tathmini msimu huu unaomalizika leo kuona ni wapi walipatia, wapi walichemsha na kisha kuchukua hatua ya kurekebisha mambo kwa msimu ujao ambao haupo jirani.

Tunaamini dosari na mkanganyiko wa ratiba, TFF na TPLB watakaa chini na kurekebisha wakati wakienda kuipanga kwa msimu mpya ili kuhakikisha mechi za Ligi Kuu Bara haziingiliani na kalenda za mechi za kimataifa kwa ngazi ya klabu, timu za taifa na hata zile za kimataifa zinazotambuliwa na Mashirikisho ya CAF na FIFA.

TFF/TPLB watambue kabisa kuna michuano mingine mbali na Ligi Kuu na Kombe la FA, kama Kombe la Mapinduzi, SportPesa Super Cup, Kombe la Chalenji na hata michuano ya kimataifa ambayo yote lazima iangaliwe kwenye ratiba ya msimu ujao. Tabia ya ratiba kupangwa kisha kupanguliwa ovyo sio tu inatibua utamu wa ligi, lakini pia inachangia kukimbiza hata wadhamini wa kujitosa kwenye ligi hiyo.

TFF ipambane mapema kupata wadhamini, ili kuifanya ligi ijayo iwe tamu zaidi kwa timu kuwa na ushindani na uwiano unaiolingana kuliko sasa zile zenye uwezo ndio zilizoonekana kutawala zaidi ya klabu nyingine. Kadhalika TFF/TPLB kuhakikisha waamuzi wanaoteuliwa na kupangwa kwa mechi za msimu ujao wanakuwa bora na makini kwa nia ya kuepuka kuharibu mechi kama ilivyotokea kwenye baadhi ya mechi za msimu huu. Maamuzi tata kama yale yaliyojitokeza Mkwakwani Tanga ama CCM Kirumba kati ya Simba na KMC ni mambo yanayoharibu taswira ya soka la Tanzania.


Share.

About Author

Leave A Reply