Friday, July 19

KRC Genk yabanwa mbavu nyumbani

0


By Eliya Solomon

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Mbwana Samatta ameshindwa kufurukuta kwenye mchezo wa Ligi Kuu Ubelgiji ambao KRC Genk imeambulia pointi moja kwa kwenda sare ya bao 1-1 dhidi ya Club Brugge.

Samatta aliyekuwa amevaliza jezi yenye mchoro wa ng’ombe wa dhahabu, amekuwa akitazamwa kwa jicho la tatu kutokana na kuongoza kwake kwenye orodha ya wafungaji lakini walibanwa vilivyo kwenye mchezo huo ambao walicheza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Luminus.

Bao la KRC Genk kwenye mchezo huo, lilifungwa na Mkongomani, Dieumerci N’Dongala anayevaa jezi namba 77 iliyokuwa ikivaliwa zamani na Samatta hapo awali.

Sare hiyo imeifanya KRC Genk kuendelea kusalia nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Ubelgiji wakiwa na pointi 34 huku wanaowafuata Club Brugge wakiwa na pointi 31.

Siku moja kabla ya mchezo wa KRC Genk dhidi ya Club Brugge, ilitangazwa kuwekwa rekodi msimu huu ndani ya klabu hiyo kwa kuuza tiketi zote za mchezo huo.

Kinachotajwa kuchochea kuuzwa kwa tiketi hizo ni kiwango chao kizuri hasa wanachoonyesha msimu huu, huku kukichangiwa na moto wa mshambuliaji wa Kitanzania Mbwana Samatta.

Baada ya mchezo huo uliopigwa juzi Jumamosi, KRC Genk wataingia tena mzigoni kwenye michuano ya Europa League kwa kuikaribisha Beikta kwenye uwanja wao wa nyumbani.

KRC Genk itacheza mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Waturuki hao kwenye mchezo wa kwanza kwa mabao 4-2 huku Samatta akitupia nyavuni mabao mawili.

Share.

About Author

Leave A Reply