Saturday, August 24

Kiunzi: Wachezaji hawa wameshikiwa mikataba yao Azam

0


Dar es Salaam. LIGI inaelekea ukingoni na kuna wachezaji ambao wanamaliza mikataba yao lakini mabosi wa timu zao wanakuwa tayari wameshaanza kufanya nao mazungumzo ya mapema ili kuhakikisha wataendelea kukipiga kwenye vikosi vyao.
Kwa upande wa Azam, wao ndiyo wamekuwa wa kwanza kuhakikisha wanawabakiza wachezaji wao nyota baada ya kuwaongezea mikataba, Yakub Mohammed, Donald Ngoma, Abdallah Kheri ‘Sebo’ na Bruce Kangwa ambao wamekuwa katika kipindi kizuri tangu wamejiunga na timu hiyo.
Lakini ghafla zoezi hilo likasimama licha ya kwamba maongezi ya mktaba mpya yalikuwa tayari yameshaanza katika ngazi ya awali.
Mwanaspoti linafahamu mabosi wa klabu hiyo walikuwa wanataka kuwabakiza nyota wao wote, lakini anayetajwa kuwa kocha wao mpya, Ndayiragije Ettiene amewaambia mabosi hao wasimamishe zoezi hilo mpaka atakapofika.
Mwanaspoti linakuletea orodha ya wachezaji ambao wanamaliza mikataba na timu hiyo, lakini kuongezewa kwa mikataba yao, kumeganda kutokana na kocha huyo ambaye anatarajiwa kujiunga mwishoni mwa msimu.

STEPHEN KINGUE
Kiungo huyu ni miongoni mwa wachezaji  bora katika eneo la ukabaji wanaocheza timu hiyo. Azam ilikuwa na mchezaji huyo msimu uliopita, lakini alipomalizana nao aliondoka.
Msimu huu alirejea dirisha dogo la usajili na tangu alipotua nchini alionyesha kiwango kizuri katika eneo la ukabaji na kuwafanya mabosi hao kuanza kumzungumzia kuhusu mkataba mpya.
Hata hivyo, mabosi wa Azam wamebidi watulie kuongeza mkataba kutokana na kocha wao anayetajwa (Etienne) kuwaambia wasiendelee na usajili wowote mpaka atakapofika.

IDD KIPAGWILE
Bila shaka hakuna mwenye maswali kuhusu uwezo wake wa kukokota mpira na chenga zake za madaha. Kazi yake uwanjani kila anayeangalia mechi za Azam anatambua.
Kipagwile anakumbukwa kwa goli lake alilofunga mwaka juzi na kuitoa Simba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na kupewa jina la ‘Mtoto Idd (Kazua Balaa)’.
Baada ya hapo hajawa na wakati mzuri kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, wakati huo huo mkataba wake ukiwa unamalizika mwishoni mwa msimu, hivyo kocha atakayepewa mikoba Azam ndiyo ameshikilia hatma ya winga huyu katika kikosi hiko.

WAZIR JUNIOR
Straika huyu alisajiliwa na Azam Juni 2017, akitokea kikosi cha Toto African baada ya kuwapiga kikumbo Yanga waliokuwa tayari wameshaanza mazungumzo na mchezaji huyo na kumfikisha hadi katika ofisi zao, lakini mwisho wa siku hawakufanikiwa kupata saini yake.
Hata hivyo, haikuwa riziki katika kikosi hicho kwani akiwa katika wakati wa maandalizi ya msimu mpya alipata majeraha yaliyomfanya akae nje takribani msimu mzima.
Msimu huu alirejea kidogokidogo, lakini bado hakupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza na kuamua kutoka kwa mkopo kwenye dirisha dogo na kutimkia Biashara United ambako amefunga magoli matatu tu.
Mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu hivyo naye anaingia katika orodha hii kwa vile hakuna maamuzi yoyote ambayo yamefanyika mpaka hivi sasa licha ya kwamba msimu unaelekea ukingoni.

ENOCK ATTA
Nchini Ghana wanaweza wakashangaa wakisikia kwamba winga huyu bado hajaweka dole gumba la kuitumikia Azam kwaajili ya msimu ujao au kukosa timu mpaka hivi sasa.
Ni mchezaji wa kikosi cha timu ya Taifa Ghana chini ya miaka 23 akiwa miongoni mwa wachezaji waliocheza mashindano yote ya vijana chini ya umri huo.
Atta ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao imeshikiliwa na hatma ya kocha ambaye atatua katika kikosi hiko.

BENEDICT HAULE
Hili ni zao la Azam ambalo limetengenezwa katika akademi yao na baada ya kuwa fiti aliamua kuondoka zake na kutimkia katika kikosi cha Mbao.
Akiwa Mbao mwaka juzi alikuwa katika kiwango kizuri hali iliyowafanya mabosi wa Azam kuhakikisha wanamrejesha mchezaji huyo nyumbani na walifanikiwa kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.
Lakini katika kikosi hiko alishindwa kuleta ushindani mbele ya Razack Abalora na Mwadini Ally, licha ya kwamba yeye binafsi amekuwa akifanya vizuri pindi anapopewa mechi.
Mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu na hajajua hatma yake baada ya mabosi wa timu hiyo kusimamishwa kufanya lolote katika usajili huku kubwa zaidi ikitajwa kwamba kikosi hicho kipo mbioni kumalizana na kipa, Jonathan Nahimana anayeichezea KMC. Ujio wa kocha mpya ndio utaamua nani anabaki na nani atafunguliwa mlango wa kutoka na kwenda kusaka maisha sehemu nyingine.

Share.

About Author

Leave A Reply