Wednesday, August 21

Kitabu cha ukaguzi vituo chapokewa

0


By Jesse Mikofu na Johari Shani, [email protected]

Mwanza. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza imetupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi na kukubali kitabu maalumu cha ukaguzi wa vituo vya polisi na lindo kipokewe kama kielelezo katika kesi ya shehena ya kilo 319 za dhahabu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Rhoda Ngimilanga baada ya kukubaliana na hoja za upande wa Jamhuri kuwa pingamizi la upande wa utetezi lililowekwa na wakili Deo Mgengeli halikuwa na nguvu kisheria.

“Baada ya kupitia maamuzi ya Mahakama za juu na kwa kuzingatia kifungu cha 192 cha mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20, Mahakama hii inatupilia mbali pingamizi na kuruhusu kitabu hicho kupokewa kama kielelezo,” alisema Hakimu Ngimilanga.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, Mahakama inaruhusiwa kupokea kielelezo chochote kitakachoisaidia kufikia uamuzi hata kama hakikuorodheshwa au kutajwa wakati wa usikilizwaji wa awali.

Baada ya uamuzi huo, kitabu hicho kilipokewa kama kielelezo cha 12 cha upande wa mashtaka, P12.

Washtakiwa katika shauri hilo ni pamoja na aliyekuwa mkuu wa oparesheni Mkoa wa Mwanza, Morice Okinda, E 6948 D/CPL Kasala, F 1331 PL Matete, G 6885 D/C Alex na G 5080 D/C Maingu.

Wengine ni G 7244 D/C Timothy, G 1876 D/C Japhet, H 4060 D/C David Kadama ambao walifikishwa mahakamni hapo kwa mara ya kwanza Januari 11 mwaka huu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kutakatisha fedha, rushwa, uhujumu uchumi, kula njama ya kutenda uhalifu katika shauri linalohusu shehena ya dhahabu na fedha taslimu Sh305 milioni.

Mabishano ya kisheria kuhusu kielelezo hicho yaliibuka baada ya wakili mwandamizi wa Serikali, Castus Ndamugoba kumwongoza shahidi wa saba katika shauri la jinai namba 1/2019 dhidi ya waliokuwa askari polisi wanane kuiomba Mahakama kukipokea kitabu hicho kama kielelezo.

Wakili Ndamugoba alifikia hatua hiyo baada shahidi huyo, mkaguzi msaidizi wa Polisi, Andason Nyonyi kuonyeshwa na kukitambua kitabu hicho kilichokuwa na saini yake kuthibitisha vituo vya polisi, ofisi za Serikali na vituo vya mafuta alivyokagua usiku wa kuamkia Januari 5, 2019.

Wakili wa utetezi, Deo Mgengeli aliweka pingamizi akidai kwamba licha ya shahidi huyo kutokuwa mtu sahihi kukitoa mahakamani kama kielelezo, kitabu hicho pia hakimo kwenye orodha ya vielelezo vilivyotajwa na Jamhuri wakati wa usikilizwaji wa awali.

Pingamizi hilo lilipingwa na wakili wa Serikali mkuu, Fredrick Manyanda aliyedai kuwa licha ya shahidi huyo kuwa mtu sahihi kutokana na jina na saini yake kuwemo kwenye kitabu hicho, Mahakama pia haibanwi kupokea kielelezo chochote hata kama hakijaorodheshwa wakati wa usikilizwaji wa awali.

Wakili Manyanda alitumia kifungu cha 192 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 pamoja na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kujenga hoja yake ndipo Hakimu Ngimilanga alipoahirisha shauri hilo ili kupata muda wa kupitia hoja za pande zote kabla ya kutoa uamuzi wake jana.

Baada ya uamuzi huo, shahidi huyo aliendelea kutoa ushahidi wake ambako aliiambia Mahakama kuwa hakukuwa na tukio lolote kubwa la kihalifu tangu alipoingia kazini Januari 4, 2019 hadi alipotoka saa 12:00 asubuhi ya Januari 5, 2019.

“Katika kila kituo cha Polisi, ofisi za umma na taasisi za Serikali pamoja na vituo vya mafuta nilivyokagua niliandika taarifa zote muhimu ikiwemo majina ya askari niliowakuta na kutia saini,” shaihidi huyo aliiambia Mahakama.

Alisema kiutaratibu, kama kungekuwa na tukio lolote kubwa jijini Mwanza, angejua ama kwa kupitia ukaguzi wake vituoni na kwenye lindo au kupitia mawasiliano ya redio ya upepo ya Polisi ambayo alikuwa nayo.

Share.

About Author

Leave A Reply