Sunday, August 18

Kimbunga Kenneth chayeyuka, lakini….

0


By Tumaini Msowoya na Kelvin Matandiko, Mwananchi

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kimbunga Kenneth kinaweza kugeuka na kurejea tena baharini kisha kikapata nguvu ya mgandamizo.

Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa TMA, Dk Agnes Kijazi amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Kijazi aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema kama kimbunga hicho kingetua nchini juzi kama ilivyotabiriwa na TMA, kingeziathiri halmashauri 11 za mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na kuwafikia zaidi ya watu 1,175,000.


Jana Mwananchi lilipata taarifa kutoka katika mikoa hiyo kuwa hadi saa 12:00 jioni hali ilikuwa shwari katika mikoa hiyo na watu walikuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kimbunga hicho kilitua juzi na kupiga Pwani ya Kaskazini ya Msumbiji.

Juzi Dk Kijazi alisema kimbunga cha mwisho kuikumba Tanzania katika mkoa wa Lindi ilikuwa mwaka 1952 wakati huo nchi ilikuwa chini ya utawala wa kikoloni.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, baadhi ya wananchi walisema wanashukuru Mungu jana kulikucha salama na maisha yakaendelea kama kawaida.

Mmoja wa wananchi wa Mtwara, Aneth Kisika alisema japo juzi alipata taharuki lakini jana aliendelea na kazi zake kama kawaida.

“Jana (juzi) ndiyo nilipata hofu sana lakini leo (jana) tumeamka salama na hali ni shwari kabisa nipo kazini na ninaendelea na shughuli zangu,” alisema Kisika.

Taarifa zinaeleza kuwa, watu waliokuwa wamejihifadhi kwenye maeneo salama walirejea kwao na wengi wao waliendelea na kazi kama kawaida.

“Hakuna mvua wala upepo, hali ya kawaida na watu wanaenda shambani, kazini, kuvua kwa sababu jana (juzi) shughuli zote zilisimamishwa,” alisema Arnold Kinaia. Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Moses Machali alisema hali ni shwali na maisha yanaendelea kama kawaida.

“Leo (jana) imekuwa kama jana (juzi) kwa maana kwamba hakuna jua na kuna wingu kidogo na maisha yanaendelea kama kawaida. Wananchi wanaendelea na shughuli zao kazi lakini kwa sababu leo ni sikukuu ya Muungano wafanyakazi hawajaenda kazini.”

“Tunamshukuru sana Mungu kwa sababu ametunusuru katika hili.” alisema.

Share.

About Author

Leave A Reply