Monday, June 17

Kigogo mzito ajitoa Yanga

0


By Charity James

WAKATI zoezi la usaili katika uchaguzi Mkuu wa Yanga likifia tamati leo Jumanne kabla ya Kamati zinazosimamia uchaguzi huo kuanika majina ya watakaopenya, kigogo mzito aliyekuwa anawania nafasi ya Uenyekiti, Lucas Mashauri inaelezwa amechomoa kuendelea na mchakato huo.

Mashauri ambaye alikuwa mmoja kati ya majina tishio katika vigogo waliochukua fomu katika kuwania nafasi ya hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Yusuf Manji kabla ya kujiuzulu mwaka juzi, inaelezwa ameshindwa kuendelea na mchakato huo kutokana na kubanwa na majukumu yake binafsi.

Taarifa ndani ya Kamati ya uchaguzi ni kwamba kigogo huyo hakutokea hata katika zoezi la usaili huku kambi yake ikidai jamaa amechomoa na hataendelea tena na uchaguzi huo.

Mbali na sababu hiyo inaelezwa kuwa kigogo huyo ameombwa na familia yake kutochukua kiti hicho kizito, lakini abaki kuwa kiongozi mwandamizi kuisaidia klabu hiyo ambayo kwa sasa inapitia katika kipindi kigumu ikikabiliwa na ukata wa kifedha tangu bilionea wao, Manji kujiuzulu.

Mwanaspoti jana Jumatatu lilimtafuta Mashauri ambapo, alishindwa kukubali au kukataa akisema taarifa kamili ataitoa mapema iwezekanavyo juu ya uamuzi wake katika mchakato huo.

“Nitatoa taarifa kamili siku si nyingi subirini mtapata usahihi wa hilo muda mfupi ujao au kesho (leo),” alisema Mashauri kwa kifupi.

Kigogo huyo kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Yanga baada ya viongozi wote wa kuchaguliwa na wale wa kuteuliwa kupitia uchaguzi uliopita kujiuzulu.

Share.

About Author

Leave A Reply