Saturday, August 24

Kidunda amuibua Snake Boy

0


By Imani Makongoro

UNAMKUMBUKA Seleman Kidunda, yule nahodha wa timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa, jamaa sasa hataonekana tena kwenye mapambano ya timu ya taifa na badala yake uongozi wa Ngumi za Wazi (OBFT), umemuombea kibali cha kucheza ngumi za kulipwa.

Uamuzi huo umepokewa kwa mtazamo tofauti na bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla aliyemwambia Kidunda kama anahitaji kuwa bora kwenye ngumi, lazima ajitoe kwelikweli kwenye ngumi za kulipwa.

Katibu Mkuu wa OBFT, Lukelo Wililo alisema, bondia huyo kwa sasa ameombewa kibali cha kucheza ngumi za kulipwa.

“Tumemuombea kibali kwa waajiri wake, Jeshi ili acheze ngumi za kulipwa, mkakati huo unakwenda vizuri na siku si nyingi ataanza kupigana kwenye ngumi za kulipwa na huku kwenye ridhaa hataonekana tena,” alisema Lukelo.

Mbali na Kidunda pia, Emillian Patrick ambaye alifuzu Olimpiki ya 2008 na Fabian Gaudence nao wameombewa vibali vya kujiunga na ngumi za kulipwa.

Baada ya uamuzi huo, Matumla aliyefahamika zaidi enzi zake kama Snake Boy alisema OBFT imeona mbali kuchukua uamuzi huo, lakini akatoa angalizo kwa Kidunda na wenzake kwenye harakati hizo.

“Ngumi za kulipwa zina tofauti kidogo na zile za ridhaa, kuanzia raundi za kucheza na baadhi ya sheria, lakini kama Kidunda na wenzake wameamua kuingia huku sina shaka kwamba watamudu, cha msingi wasiwe waoga,” alisema Matumla.

Alisema ngumi za kulipwa zinahitaji uvumilivu, kujituma na mazoezi ya kutosha.

“Kinyume na hapo utakwama njiani, hivyo Kidunda hana budi kupambana kwelikweli na kwa umri wake, uwezo wake aliouonyesha ngumi za ridhaa ni wazi atafikia levo ya juu.”


Share.

About Author

Leave A Reply