Sunday, August 18

Kesi ya Yanga uchaguzi yaiva, Mahakama kutoa hukumu Mei 3

0


By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Mei 3, mwaka huu kutoa hukumu katika kesi ya kupinga uchaguzi wa Klabu ya soka ya Yanga, iliyofunguliwa na wajumbe wawili wa klabu hiyo.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka  2019, ilifunguliwa, Januari 11, 2019, na wanachama wawili wa Klabu ya Yanga, ambao ni Juma Magoma na Athman  Nyumba dhidi ya bodi ya wadhamini wa klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Katika kesi hiyo, wadai hao wanapinga kufanyika kwa uchanguzi Mkuu wa Klabu hiyo, kwa madai kuwa unakwenda kinyume na katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010, ibara ya 7.

Hukumu hiyo inatarajia kutolewa kwa upande mmoja bila wadaiwa kuwepo baada ya kushindwa kuitikia wito wa kufika mahakamani hapo.

Uamuzi huo, umetolewa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Janeth Mtega, baada ya kusikiliza ushahidi wa wajumbe hao dhidi ya wadaiwa hao.

Wakitoa ushahidi wao, jana mbele ya Hakimu Mtega, wadai hao Magoma na Nyumba, walidai kuwa wanaiomba Mahakama ya Kisutu kutupilia mbali matumizi ya kadi za kielekroniki zilizotolewa na benki ya CRDB na benki ya Posta, zisitumike katika uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.

Wakiongozwa na wakili wao, Said Aziz, wadai hao wanaiomba mahakama hiyo kuwa kadi hizo za benki ya CRDB na benki ya Posta zisitumike pia katika chaguzi zote za klabu ya Yanga.

Nyumba na Magoma waliendelea kueieleza mahakama hiyo kuwa, kadi zinazotakiwa kutumika kwa sasa katika chaguzi zote za klabu ya Yanga ni ile kadi ya kitabu (kadi ya vitabu) ambayo inatambuliwa na katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010, ibara ya 7.

Hakimu Mtega baada ya kusikiliza mashahidi hao wawili, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 3, mwaka huu atakapotoa hukumu dhidi ya kesi hiyo.

Itakumbukwa kuwa, tangu kesi hiyo ilipofunguliwa wadaiwa hawajawahi kufika mahakamani licha ya kupelekewa wito wa mahakama mara kadhaa na hata kutangazwa gazetini.

Kutokana na hali hiyo, upande wa wadai kupitia kwa wakili wao Daudi Mzeri, April 8, 2019, uliiomba mahakama hiyo iamauru kesi hiyo iendelee kusikilizwa upande mmoja, akidai kuwa imekuwa vigumu kwa mdaiwa huyo kupoikea hati ya wito iliyotolewa na mahakama.

Wakili Mzeri alidai kuwa licha ya Mahakama hiyo kuamuru, Bodi ya wadhamini wa Klabu ya Yanga kutangazwa katika gazeti la Uhuru kama njia ya wito wa kufika mahakamani hapo, bado imekuwa vigumu kufika mahakamani hapo kusikiliza shauri hilo.

Kabla ya wadai kutoa ushahidi wao leo, kesi hiyo imeshatajwa mara tatu kwa maana ya Februari 11, Machi 11 na April 8, bila wadaiwa kufika mahakamani kusikiliza shauri hili, hali iliyopeleka mahakama hiyo kukubaliana na maombi ya upande wa madai ya kusikiliza shauri hili upande mmoja.

Wakili Mzeri alidai kuwa mdaiwa wa pili katika shauri hilo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), alitangazwa Februari 8, 2019 kupitia gazeti la Uhuru, huku mdaiwa wa kwanza, yeye hajatangazwa gazetini kwa sababu alipokea wito wa mahakama, lakini hakufika mahakamani.

Uchaguzi mkuu wa klabu hiyo ulipangwa kufanyika Januari 13, 2019, kwa lengo la kujaza nafasi mbalimbali zilizoachwa wazi, lakini ulishindikana kutokana na kufunguliwa kwa kesi hiyo.

Katika madai yao Magoma na Nyumba wanapinga kufanyika kwa uchaguzi huo kwa madai kuwa unakwenda kinyume na katiba ya Klabu ya Yanga ya mwaka 2010 ibara ya 7.

Ibara hiyo inaelezea utaratibu wa uanachama ndani ya Klabu ya Yanga ambao, kwanza ni kutuma maombi, ambapo maombi hayo yatapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, ambaye baaade yatajadiliwa na kamati tendaji.

Pia, ibara hiyo, inaelezea kuwa maombi hayo yataambatana na fomu namba YASC/U, ada ya uanachama ambayo ni Sh 12,000 pamoja ana ada ya kadi ambayo ni Sh 2000.

Pia, wanadai kuwa kuna taarifa za kuwepo kwa wanachama wenye kadi feki za kieletroniki ambazo zina saini na mhuri ambazo zinasambaa kwa baadhi ya wanachama, ambazo zinaonyesha kuwa zimetolewa na benki ya CRDB pamoja na benki ya Posta.

Wanadai kuwa kadi hizo zinazodaiwa kuwa ni kadi za uanachama wa Klabu ya Yanga, zikiwa na picha za wamiliki ambazo sio mali ya klabu hiyo.

Hivyo wanapinga matumizi ya kadi hizo kutumika katika uchaguzi huo wakidai kuwa kwa namna yoyote ile haziwezi kuwa na uthibitisho wa uanachama wa Yanga, kwa kuzingatia kwamba, wahusika wa kadi hizo, hawakupitia utaratibu ulioanishwa katika ibara ya 7 ya mwaka 2010 ya klabu ya Yanga.

Share.

About Author

Leave A Reply