Saturday, August 24

Kenya yataka mjadala wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mapambano bidhaa bandia

0


By Nasra Abdallah,Mwananchi nabdallah mwananchi.co.tz

Nchi ya Kenya imetaka kuitishwa kwa mjadala na kujadili kuhusu tatizo la bidhaa bandia katika nchi za Afrika Mashariki.

Ushauri huo umetolewa leo Jumanne,  Mei  21 ,2019, na Mkurugenzi wa shirika la ushindani la nchini Kenya, Steven Mutoro, katika ziara yao ya siku tatu ya  wajumbe kutoka Shirika la hilo na wale wa wakala wa ushindani nchini Kenya, wakiokuja kujifunza namna Tume ya ushindani hapa nchini(FCC)inavyofanya kazi zake.

Mutoro amesema tatizo hilo ni kubwa na hakutakuwa na maana kila nchi  ikijifungia yenyewe kutafuta suluhu ya kupambana nalo na badala yake nchi hizo zinatakiwa kuungana.

‘Suala la bidhaa bandia halina mipaka, linaathiri kila nchi na bila ushirikiano wa pamoja hatuwezi kufanikiwa katika vita hii na ndio maana kama Kenya tumeamua tuje Tanzania ili tuweze kubadilishana uzoefu wa nini cha kufanya katika mapambano hayo ambayo ni tatizo pia la kidunia,”amesema Mutoro.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wa Wakala wa  kuzuia bidhaa bandia  nchini Kenya(ACA), Flora Mutahi, amesema inasikitisha kuona asilimia 40 ya soko la bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vilivyopo nchi  za Africa Mashariki linapotea kutokana na uwepo wa bidhaa bandia.

Mutahi amesema bidhaa feki mbali ya kuwa na athari kiuchumi ikiwemo viwanda kufa na wawekezaji kukimbia, pia hupoteza ajira za wazawa,husababisha athari kwa afya ya watumiaji na hivyo kuchangia kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

“Tuna kila sababu nchi hizo za Africa Mashariki kuungana la sivyo tutajikuta hata hao wawekezaji tunaotumia nguvu nyingi kuwashawishi  waje watukimbie au hawaji kabisa kwa kuwa tumeshindwa kuvilinda viwanda vyetu na bidhaa bandia zinazoingizwa,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa FCC, Profesa Humphrey Mushi, amesema bado kuna tatizo kubwa la uelewa miongoni mwa jamii kuhusu bidhaa bandia huku wengi wakiponzwa na kuuziwa kwa bei rahisi ukilinganisha na zile halisi ambazo bei yake huwa huu.

“Tutaendelea kutoa elimu bila kuchoka kwa watumiaji ikiwemo kupitia nyie waandishi ambayo mnawafikia watu wengi kwa wakati mmoja.

” Pia Serikali katika mipango yake imeshaanza kutekeleza mipango wa kupambana na bidhaa hizo  huko zinapotengenezwa kwa kuwa na ofisi na ushirikiano wa taasisi za nchi husika zinazopambana na bidhaa bandia,”ameeleza Profesa Mushi.

Share.

About Author

Leave A Reply