Friday, August 23

Kauli ‘tata’ za mawaziri zilizotikisa bungeni

0


By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Kama kuna majibu na maelezo yaliyotolewa bungeni na kutikisa Bunge tangu lilipoanza vikao vyake Aprili 2, ni yale yaliyotolewa na naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji na naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Wakati Dk Kijaji akisema Zanzibar ikikopa inayolipa ni Serikali ya Tanzania, Nyongo kauli yake kuhusu Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuwa mwanachama wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kutoa mfano wa vyama vya soka vya mikoa kuwa wanachama wa TFF, uliwafanya wabunge wa Zanzibar kumjia juu wakidai ameifananisha nchi hiyo na mkoa.

Kauli hizo zilitolewa ufafanuzi na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na ya Dk Kijaji ikiwekwa sawa na mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ambaye aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali.

Sakata la ZFA na TFF liliibuliwa na mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, kuhoji mgawo wa ZFA kutoka Fifa kwenda TFF. Katika majibu yake, Nyongo alisema: “Mfano Marekani, pale California wana chama cha mpira na majimbo mengine ila majimbo yote ni wanachama wa chama cha mpira wa miguu cha Marekani.”

Khatib akijibu taarifa ya Nyongo alisema ZFA si mwanachama wa TFF, ni chombo huru huku mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Najma Murtaza Giga naye akiomba taarifa akitaka Nyongo aeleza sababu za kuifananisha Zanzibar na mkoa.

“Nyongo amesema Zanzibar ni sawa na mikoa mingine, aweke sawa, maana Zanzibar ndani ya Tanzania ni nchi ila nje ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Giga ambaye pia ni mwenyekiti wa Bunge.

Katika maelezo yake, Dk Tulia alisema Nyongo alizungumzia chama cha michezo si Zanzibar kama mkoa na kutaka wabunge ambao hawajaelewa wakasikilize taarifa za kumbukumbu za Bunge.

Kauli hiyo iliwanyanyua wabunge wengi wa upinzani na kumpinga Dk Tulia. Katika vuta nikuvute hiyo mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alitolewa nje ya Bunge huku Khatib akisusa kuendelea kuchangia kwa sababu ya Zanzibar kuitwa mkoa.

Maelezo yaliyotolewa na Dk Kijaji yalimduwaza waziri wa zamani katika wizara hiyo, Saada Mkuya.

Dk Kijaji alikuwa akijibu hoja ya mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea aliyetishia kutoa shilingi akitaka Serikali itamke ni lini itapeleka bungeni muswada wa kubadilisha Katiba na sheria ili Zanzibar iruhusiwe kukopa na kuendesha miradi yake mikubwa kama ujenzi wa bandari na uwanja wa ndege.

Dk Kijaji alisema: “Namuomba Kubenea aiachie shilingi. Dhamira ya Serikali ni njema kuhakikisha miradi yote mikubwa inatekelezwa pande zote mbili za Muungano.”

Kuhusu mkopo alisema: “Hili ni jambo la kikatiba, mchakato wake umeanza na yapo mambo tunajadiliana, tunapoomba Zanzibar ikope moja kwa moja nani wa kulipa mkopo huo? Hili ni jambo la Muungano. Serikali mbili zinakaa na kujadiliana.”

Wakati Dk Kijaji akitoa maelezo hayo, Dk Mkuya alishika kichwa kwa mikono miwili na kuangalia huku na huko na wakati mwingine kuziba mdomo akiashiria kutokubaliana naye na alipoulizwa nje ya viwanja vya Bunge sababu za mshangao wake alisema: “Hicho kitu (Zanzibar kukopa) hakipo. Kila kitu kimewekwa vizuri katika sheria tunapokopa… Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikilipa maana yake Zanzibar imelipa.”

Mbunge huyo wa Welezo (CCM), alisema amemshangaa waziri kwa kutoa kauli zenye mkanganyiko akidai wanaozisikia nao wanapata mchanganyiko.”

Chenge aliweka suala hilo sawa: “Naomba tuweke rekodi sawa. Nadhani Naibu Waziri wa Fedha ameteleza tu ulimi. Dhamana inatolewa kwa mujibu wa Katiba na sheria ya mikopo, dhamana na misaada ya mwaka 1974 ambayo juzi tumeifanyia marekebisho. Dhamana inatolewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatuna Serikali ya Bara. Nimeona tunyooshe hilo ni suala la msingi sana.”

Share.

About Author

Leave A Reply