Monday, March 18

Kanuni mpya za mafao zawaibua wastaafu wajao

0


By Ephrahim Bahemu na Burhani Yakub, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Swali la nani atafaidika na nani ambaye hatafaidika na kanuni mpya za sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii za mwaka 2014 huenda halijawa na majibu ya moja kwa moja kwa watu wengi.

Hivi karibuni uliibuka mjadala baada ya kutangazwa kwa kanuni mpya za sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2014 ambazo pamoja na mambo mengine zilielekeza kuwa wastaafu katika mifuko yote watalipwa mkupuo wa asilimia 25 na asilimia 75 watakuwa wakilipwa kama pensheni ya kila mwezi.

Serikali inasema kanuni hizo zitaboresha maisha ya wastaafu, lakini wafanyakazi wanakosoa kwa kusema ni kandamizi na wamezipokea kwa mtazamo hasi hivyo zitashusha morali yao ya kazi na ufanisi.

Joseph David, ambaye ni mtumishi wa Serikali, alisema kanuni zinafaa kwa wastaafu ambao hawakuwa na mipango ya biashara baada ya kustaafu, lakini kwa wenye mipango ni kikwazo.

Alisema kuna watu wengi maisha yao yamekuwa bora zaidi baada ya kustaafu kwa kuwa walitumia mafao yao ya mkupuo kufanyia biashara na sasa wanaendelea vizuri, lakini wapo ambao waliutumia vibaya na sasa hali zao ni taabani.

David (51) alisema ni kosa kwa Serikali kuona kuwa wastaafu wote hawana uwezo wa kusimamia fedha wanapostaafu.

Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Jones Majura alisema kwa sasa wanafanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wanachama wao juu ya uwekezaji hata kabla ya kustaafu.

“Ndiyo maana tunasema watu wapewe pesa zao waweze kuwekeza na miongoni mwa vitu tulivyovipigania na tukafanikiwa ni kuruhusu mafao mkupuo yawe amana ya kuombea mkopo, lakini ikiwa asilimia 25 sio rahisi kufanya uwekezaji baada ya kustaafu,” alisema Majura.

Alisema kwa kikokotoo cha sasa endapo mfanyakazi atafariki dunia kabla ya kufikia miaka 12.5 baada ya kustaafu, ataacha fedha zake nyingi lakini angepewa kama mkupuo zingewezesha kuinua hali za familia yake.

Wakizungumza mkoani Tanga, baadhi ya walimu wanaotarajiwa kustaafu kuanzia Januari hadi Desemba, 2019 walisema mjadala unaoendelea kuhusu mafao unawaathiri kisaikolojia kwa kuwa kama utapitishwa watakuwa waathirika wa kwanza wa sheria hiyo.

Walitoa malalamiko hayo jana wakati ufunguzi wa semina ya kuwaandaa walimu wanaotarajia kustaafu kuanzia iliyoandaliwa na kitengo cha wanawake cha Chama cha Walimu (CWT), Wilaya ya Tanga.

Jumla ya walimu 37 wanachama wa CWT wanatarajiwa kustaafu kazi mwakani na kama mapendekezo ya kulipwa mafao kwa mkupuo kwa asilimia 25 yatapitishwa, utekelezaji wake utawahusu.

Mwalimu Abdullah Uledi alisema, “Nilijaribu kukaa na mtaalamu mmoja akanipigia hesabu kwa kufuata kanuni ya kikokotoo kipya nikabaini sitapata kitu, yaani hela ninayoapata itakuwa ndogo, haitanisaidia, ni maumivu matupu.”

Mwenyekiti wa kitengo hicho, Dianarose Bendera alisema, “Kwa kweli jambo hili ni zito mno, kuna hatari mkaona baadhi yetu tunaanguka ghafla kwa sababu ya kuwaza sana tutaendeshaje maisha nje ya kazi.”

Katibu wa CWT Wilaya ya Tanga, Victor Ntumbo alisema mabadiliko ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii hususani PSSSF kwa sehemu kubwa hayamsaidii mwanachama wa iliyokuwa PSPF.

Ofisa Mkuu wa PSSSF Mkoa wa Tanga, Nyemo Chomola aliwasihi wastaafu hao watarajiwa kuvuta subira katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na watumishi wanaotarajia kustaafu baada ya kutangazwa kwa mapendekezo ya kikokotoo cha asilimia 25 kwa mafao ya mkupuo na 75 ya pensheni ya kila mwezi.

Share.

About Author

Leave A Reply