Saturday, August 17

Kampeni ya kumsaka Azory yazinduliwa

0


By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeibua matumaini mapya kwa wanahabari nchini, baada ya jana Jumatatu Aprili 29,2019 kuzindua rasmi ukurasa wa kukusanya maoni na saini za wananchi wanaoshinikiza umuhimu wa kumtafuta hadi apatikane Azory Gwanda.

Azory ni mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani ambaye Novemba 21, 2017 alitoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana  ambapo mpaka sasa hajapatikana.

MCT imezindua kampeni hiyo kupitia tovuti ya Avaaz, jukwaa linaloendesha harakati za uhamasishaji wa jambo au madai unaoanzia ngazi ya jamii, kitaifa hadi kimataifa lengo kuu ikiwa ni kuonyesha unyeti wa kumsaka hadi apatikane mwandishi huyo.

Tayari takribani ya wananchi 45 wameingia na kusaini katika jukwaa hilo huru linalounganisha hisia za watu mbalimbali katika hitaji la upatikanaji wa Azory.

Malengo ya ukusanyaji na saini hizo ni kutuma ujumbe kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania inayohusika na usalama wa raia nchini.

Azory alichukuliwa na watu waliotumia gari aina ya Toyota Land Cruiser na kumpeleka kusikojulikana ambapo mkewe alidai alichukuliwa na watu wasiojulikana.

Uzinduzi wa kampeni hiyo #WhereisAzoryGwanda #YukoWapiAzoryGwanda, inafanyika ikiwa ni siku chache zimepita tangu MCT ilipozindua Ripoti ya Hali ya Vyombo vya Habari Tanzania 2017/18, inayoonyesha kiwango cha juu cha uwoga wa kuandika habari za kuikosoa Serikali.

Katika tukio hilo, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mkajanga aliahidi kuanzisha kampeni ya kumsaka mwanahabari huyo.

Kajubi alisema anashangazwa kuendelea kusikia baadhi ya kauli za viongozi wa serikali, zinazokatisha tamaa katika juhudi za kumtafuta mwandishi huyo.

“Tunaambiwa tusiulize waandishi wa habari wakipotea

wanakwenda wapi. Kiongozi anasema waandishi wakipotea au kupotezwa tusiulize. Anasema kwa sababu watu wengi sana kule wamepotea, badala ya kusikitisha, anatumia hoja hiyo kama kihalalisho cha watu wengi wakipotea wasiuliziwe, kwa hiyo waendelee kuotea?” alihoji Kajubi.

Wakati kampeni hiyo ikianza, tayari Azory ameingia kwenye historia ya kitabu cha habari za uchunguzi ukanda  wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, kiitwacho ‘Southern African Muckraking – 300 Years Of Investigative Journalism Which Has Shaped The Region’, kilichozinduliwa nchini Afrika Kusini.

Share.

About Author

Leave A Reply