Friday, July 19

Kaheza, Mkomola waamua kupotezea Msimbazi

0


By OLIPA ASSA

NGUVU ya kiuchumi za Klabu za Simba na Yanga zinachangia kuwapa ugumu wachezaji wanaokaa benchi katika klabu hizo kusaka timu zitakazowapa nafasi ya kucheza.

Kupitia usajili wa dirisha dogo uliofunguliwa Novemba 15, baadhi makocha na viongozi walishangazwa na wachezaji hao wa Simba na Yanga licha ya kukaa benchi lakini wamekataa ofa za kuchezea klabu nyingine.

Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto ameliambia Mwanaspoti amestajabishwa na wachezaji walioonja mafanikio ya Simba na Yanga kugoma kuondoka kwa hiari na kusubiri kuondolewa kwa aibu.

Wagosi walikuwa katika mazungumzo na straika wa Simba, Marcel Kaheza, lakini Mguto alisema yalikwama baada ya mchezaji huyo kutoonyesha dalili ya kuwa tayari kuondoka.

“Umri ni kila kitu kwenye soka, mfano Kaheza ana muda mwingi wa kucheza, kukaa Simba ambako hachezi ni kama kujipotezea muda wake ama pesa anaweza kuvuna baada ya kuonyesha kiwango cha juu,” alisema.

Alipoulizwa Kaheza anaenda timu gani baada ya Simba kumtangaza kwenda kwa mkopo! Alijibu; “Bado sijafikia maamuzi na timu ambazo zinahitaji huduma yangu, sina haraka sana na hilo kama ni mazoezi bado nafanya na Simba.”

Yohana Mkomola hapati nafasi Yanga na tayari alikuwa anahusishwa kutua Namungo ya Ligi Daraja la Kwanza, lakini anaonyesha hana utayari kukubaliana na uhalisia huo badala yake alidai bado yupo sana Jangwani.

“Nafanya mazoezi na timu yangu ya Yanga ni kweli sipati nafasi, ila ipo siku nitacheza ligi bado ni ndefu,” alisema Mkomola.

Naye Kocha wa Mbao FC, Amri Said alikazia alichokizungumza Mguto kuwa, nyota wengi wakipita Simba na Yanga hawapendi kukubali changamoto ya kusaka maisha pengine.

“Tulimhitaji kipa wa Simba, Said Mohamed ‘Nduda’ na kumhakikishia atacheza katika kikosi cha kwanza, ajabu bado anakaa benchi mpaka sasa na hayupo kwenye Michuano ya Caf, unaweza kuona namna wanavyojipotezea muda wao badala ya kutengeza wanadidimiza ndoto zao,” alisema.

Nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema akitazama nyota wengi waliopo klabu kubwa anawaona wanapoteza muda wa kuvuna mabilioni waliokalia miguuni kwao.

“Kuna haja ya kuwapa elimu, kucheza Simba na Yanga haina maana ndio wamefika mwisho, wapo wachezaji ambao siwataji majina ndani ya klabu hizo, laiti wangejua ukubwa wa vipaji vyao basi tungewasikia anga za kina, Mbwana Samatta na Simon Msuva,” alisema Mogella ambaye enzi zake alikuwa matata sana katika ufungaji.

Kuna wachezaji wengi katika klabu za Simba na Yanga ambao mpaka sasa hawajapata nafasi ya kutosha katika vikosi vya kwanza na hawana matumaini ya kufanya hivyo, lakini hawataki kuhama.

Share.

About Author

Leave A Reply