Friday, August 23

Kagere akili yote ni ubingwa wa Ligi Kuu hakuna kingine

0


By Thomas Ng’itu

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere amehamishia hasira zake katika Ligi Kuu baada ya klabu yake kuondolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ilitolewa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1 na kukatisha safari yao ya kuendelea kuwepo katika mashindano hayo na kugeukia katika Ligi Kuu.

Kagere alisema yaliyotokea katika Ligi ya Mabingwa ni historia na hivi sasa akili yao wameigeuzia katika Ligi Kuu kuhakikisha wanamalizia kile ambacho walikibakiza.

“Tulichokipata katika Ligi ya Mabingwa hivi sasa ni historia tayari, kikubwa hivi sasa tunachokiangalia ni Ligi Kuu, tunapambana kuhakikisha tunachukua ubingwa,” alisema mshambuliaji huyo mwenye magoli 16 sawa na Salum Aiyee wa Mwadui Fc.

Kagere aliongeza kwamba licha ya kutolewa katika hatua ya robo fainali na Mazembe, anaimani wamefanikiwa kupata kitu kikubwa na wanajipanga kwaajili ya msimu ujao.

“Nina furaha ya kuwa katika kikosi kilichopambana muda wote katika Ligi ya Mabingwa, nawapongeza wachezaji wenzangu na benchi la ufundi pamoja na bosi wetu ‘Mo’, inabidi tujipongeze kwa hapa tulipofika,” alisema.

Kagere amekuwa na kiwango kizuri tangu alipojiunga na Simba msimu huu baada ya kufanikiwa kufunga mabao 29 katika mashindano yote aliyoshiriki baada ya kufunga 16 katika Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa 6, Kagame Cup 4, Mapinduzi Cup 2 na Ngao ya Jamii 1.

Share.

About Author

Leave A Reply