Monday, July 22

Jinsi viziwi wanavyotoa huduma nzuri mgahawa wa kitalii Iringa

0


Iringa. Kwa mteja anayeingia kwa mara ya kwanza mgahawa wa Neema Craft Café mjini Iringa anaweza kushangazwa na baadhi ya mambo ambayo si ya kawaida.

Alama za mawasiliano na karatasi itakayomtaka aandike mahitaji yake ya vyakula na vinywaji ni maarufu zaidi kuliko mhudumu kukuuliza unachotaka.

Hadi kufikia hatua hiyo ya kuandika, mteja atakuwa hajaangaza macho mgahawani kusoma baadhi ya maandishi yanayoelezea aina ya mgahawa huo na wahudumu wake.

Ni mgahawa ambao wahudumu wake ni viziwi, wasioweza kumsikia au kumwambia lolote mteja anayefika sehemu hiyo kupata huduma zaidi ya kuwasiliana naye kwa ishara.

Lakini, wahudumu hao ni watu wakarimu na wachangamfu kwa wateja.

Neema Cafe Craft, ambayo iko katikati ya mji wa Iringa, imepangwa vizuri na hivyo kuwa na mandhari nzuri inayonogeshwa na huduma nzuri ya wahudumu hao. “Naweza kusema mgahawa huu umejitangaza zaidi nje ya nchi kuliko hata hapa kwetu Tanzania,” anasema msimamizi wa Neema Cafe, Riziki Mghimba.

“Idadi kubwa ya wageni kutoka Ulaya na Afrika wanamiminika kupata huduma zetu. Wahudumu wetu wote ni viziwi na hawazungumzi, lakini ni watu waliosoma na wanaelewa kila kitu isipokuwa wanashindwa kusikia na kuzungumza tu.

“Hivyo njia kuu ya mawasiliano baina yao na wateja ni ishara na maandishi.”

Kwenye meza kuna tangazo linaloeleza kuwa wahudumu wa mgahawa ni viziwi.

“Mteja akifika tu, mhudumu anakwenda kumpa karatasi ambayo mteja anaandika mahitaji yake yote, kisha mhudumu anasoma na anaanza utaratibu wa kumpa huduma ya alichoagizwa,” alisema Riziki alipozungumza na Mwananchi katika mgahawa huo.

Alisema wazo la kuwekwa mgahawa huo ambao ni sehemu ya miradi ya Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruaha mkoani Iringa lilianzishwa na mmishenari aliyekuwa na ulemavu wa miguu.

“Nia yake ilikuwa ni kuwasaidia watu wenye ulemavu waweze kuajiriwa na kujikimu kimaisha baada ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari katika shule ya kanisa hilo.

“Kanisa lina shule ya msingi ambayo ni ya viziwi, lakini watoto wakawa wanasoma wanamaliza elimu yao na wale wanaobahatika kuendelea na sekondari walifanya hivyo, ila sasa wale wanaoishia darasa la saba wanarudi kwenye jamii,” alisema.

“Wakirudi huko elimu ile haiwasaidii kwa lolote kwa sababu jamii haiwapokei na kama itawapokea, haiwezi kushirikiana nao kulingana na elimu waliyoipata.

“Hapo ndipo mmishenari anayeitwa Susie Hart alipotoa wazo kwa uongozi wa kanisa kuanzisha kitu kitakachowasaidia kujikimu kimaisha watu wenye ulemavu badala ya kuombaomba mitaani.”

Alisema moja ya miradi hiyo ni mgahawa huo ambao ukiacha viziwi, hauajiri watu wengine wenye ulemavu unaoweza kuwazuia kuzunguka mgahawani kuhudumia.

Mradi mwingine ni nyumba ya wageni ambayo pia huhudumiwa na walemavu.

Uzoefu wa hali hiyo

Mteja kutoka Ujerumani, Mie Horiuchi Strunden alisema mara nyingi akiwa kwenye utalii na masuala mengine ya kikazi Nyanda za Juu Kusini hupenda kufikia hapo kutokana na huduma nzuri za chakula na malazi.

“Awali nilipata shida kidogo kuwasiliana na hawa watu kwani sikujua kama ni viziwi, lakini baadaye nikawazoea,” alisema Strunden.

“Nafurahia namna walivyo wakarimu na ni wachangamfu sana. Pia napenda kwa vile najifunza lugha ya ishara kwa kuwa ukiingia ndani unaona kwenye kuta wamechora signs (alama) tofauti ambazo zinatumiwa na viziwi katika mawasiliano.

“Lakini pia wana chakula kizuri na ni nadhifu sana hawa watu.”

Mkazi wa Iringa Mjini, Catherine Shembilu alisema hupendelea kuwapeleka wageni wake katika mgahawa huo kutokana na hadhi ya huduma zake.

Catherine alisema pia anajisikia kuwachangia wahudumu hao ili wapate riziki.

“Pia napenda utaratibu wao, si mgumu kabisa,” alisema.

“Ukifika hapa unaenda kaunta unapewa karatasi unarudi mezani kwako, mhudumu anakufuata basi unaandika unachohitaji, halafu unampa mhudumu huyo basi wanakuandalia chakula.”

Share.

About Author

Leave A Reply