Friday, March 22

Jaji ataja ukatili wa ngono ofisi za umma, binafsi

0


Mwanza. Wakati vumbi la tuhuma za ngono katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) halijapoa, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Agnes Bukuku ametaja maeneo ya kazi hasa maofisini kuwa eneo mojawapo lenye vitendo vya ukatili wa kingono unaotokana na matumizi mabaya ya madaraka.

Akizungumza juzi alipokuwa akiendesha shughuli za kimahakama (moot court) kwa wanafunzi wanaosomea sheria katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) jijini Mwanza, Jaji Bukuku alisema matumizi mabaya ya madaraka ya kuomba rushwa ya ngono yanaathiri utendaji na ufanisi katika baadhi ya ofisi za umma na binafsi nchini.

Alisema baadhi ya watu wenye mamlaka serikalini, utawala wa sheria na waajiri wanatumia nafasi zao kuomba na kupata rushwa ya ngono kama njia ya kuwapa nafuu wanaofika kwenye maeneo yao ya kazi kwa masuala mbalimbali.

“Licha ya kushusha utu, vitendo hivyo ni vya kijinai na ni kinyume na kifungu cha 329 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007,” alisema Jaji Bukuku.

Shughuli hiyo ya kimahakama ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupiga vita vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia iliandaliwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (Tawja) kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (Wildaf).

Mmoja wa wanafunzi waliohudhuria shughuli hiyo, Emmanuel Mtawa alisema licha ya kuelimika imewapa mwanga kuhusu vitendo vya rushwa ya ngono maofisini na kuwaomba wananchi kufanya lililo ndani ya uwezo wao kukabiliana navyo ili kuvikomesha

Tuhuma za ngono UDSM

Novemba 27, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, mhadhiri wa UDSM, Dk Vicencia Shule alimuomba Rais John Magufuli kuingilia kati vitendo vya rushwa ya ngono chuoni hapo, muda mfupi baada ya kiongozi huyo kufika kuzindua maktaba iliyojengwa kwa msaada wa Serikali ya China.

“Baba Rais Magufuli umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM. Nilitamani nikupokee kwa bango langu, lakini ulinzi wako umenifanya ninyamaze, nasubiri kutoka kwako maana wateule wako naamini ni waadilifu watakuambia ukweli,” aliandika Dk Shule.

Hata hivyo, siku chache baadaye mhadhiri huyo aliitwa na kuhojiwa na kamati ya maadili ya chuo hicho na hadi sasa hatima ya sakata hilo bado haijafahamika.

Share.

About Author

Leave A Reply