Saturday, August 24

Jafo: Hujuma chanzo moto kuteketeza sekondari ya Ashira

0


By Florah Temba, Mwananchi [email protected]

Moshi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo amesema moto ulioteketeza mabweni mawili ya ghorofa ya shule kongwe ya Sekondari ya Wasichana ya Ashira umesababishwa na hujuma.

Kutokana na hujuma hizo, Jafo amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina na kwa haraka na watakaobainika kuhusika na tukio hilo wachukuliwe hatua za kisheria.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Mei 25, 2019  baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea hali halisi ya uharibifu.

Mei 24, 2019 moto uliteketeza mabweni ya shule hiyo na kusababisha uharibifu mkubwa wa vifaa vya wanafunzi na vingine vilivyokuwa kwenye mabweni hayo. Moto huo ulitokea asubuhi wakati wanafunzi wakiwa madarasani.

“Tukio hilo la moto halikusababishwa na umeme inaonekana ni  hujuma ya makusudi. Kuna mtu au watu  wenye nia mbaya na wanafunzi wa Ashira.”

“Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuendelea kuchunguza endapo itabainika wowote waliofanya hivyo watachukuliwa hatua,” amesema Jafo.

Amesema wataalam kutoka ofisi yake watafika katika shule hiyo kufanya tathimini na kutoa taarifa nini ambacho kinapaswa kufanywa katika mabweni hayo.

“Nimepata fursa ya kutembelea miundombinu ya shule mabweni yameharibika hasa bweni moja la chini limeharibika lote, bado tuna kazi kubwa ya kufanya.”

“Kuanzia kesho muda wowote nimeagiza timu yangu kutoka Tamisemi itakuwa hapa kufanya tathmini nini kifanyike, ni gharama kiasi gani cha fedha kinahitajika, lengo likiwa ni kuhakikisha tunaikarabati vizuri shule hii,” amesema Jafo.

Naibu katibu mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Avemaria Semakafu amesema  kulingana na mazingira ya tukio hilo, inaonyesha wazi kuwa ni hujuma.

“Katika tukio hili yameungua mabweni mawili, moja vyumba viwili lakini la pili chumba kimoja. Haiwezekani bweni hili na lile vyumba vya katikati vyote  viwake kwa wakati mmoja, inaonekana kuna namna,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply