Wednesday, August 21

Ilichokisema NEMC kuhusu mifuko ya plastiki

0


By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC)  limesambaza watendaji wake nchi nzima kuhakikisha utekelezaji wa kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki unafanyika kikamilifu kuanzia Juni Mosi, 2019.

Aprili 9 2019 bungeni jijini Dodoma Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa  alitangaza marufuku hiyo na kubainisha kuwa mifuko hiyo haitakiwi kutumika ifikapo tarehe hiyo.

Akizungumza leo Jumatano Mei 29, 2019 katika semina ya  wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari  meneja wa uzingatiaji na utekelezaji wa sheria wa baraza hilo, Dk Madoshi Makene amesema katika Mkoa wa Dar es Salaam, wenye kata 97, kila kata itakuwa na maofisa wawili wa baraza hilo.

Amesema maofisa hao wa Dar es Salaam  na mikoani ambako watakuwa wawili kila Mkoa watashirikiana na watendaji wa  kata kwa ajili ya kusimamia vyema utekelezaji wa sheria na kanuni za katazo hilo.

“Tumeweka watendaji wawili katika mikoa yote isipokuwa Dar es Salaam. Maofisa hawa watavaa majaketi maalumu ili watambulike kwa urahisi,” amesema Dk Makene.

Mwanasheria huyo amesema mifuko inayotumika kuwekea sabuni ya unga katika maduka mbalimbali na kuuzwa kuanzia Sh 300 na kuendelea haitaruhusiwa kuanzia Juni Mosi.

Dk Makene amesema kutakuwa na magari maalumu yatakayopita kwenye maeneo mbalimbali kutangaza kuhusu katazo la matumizi ya mifuko hiyo na hatua iliyofikiwa hadi sasa.

Akizungumzia kuhusu kanuni za katazo hilo mwanasheria wa NEMC, Manchare Heche amewataka Watanzania kushirikiana na Serikali katika mchakato huo,  akiwaonya kuhusu utupaji hovyo wa vifungashio vya plastiki vilivyoruhusiwa.

“Endapo mtu akiwa anakula korosho au mkate yupo katika gari kisha akakitupa kile kifungashio  atapigwa faini ya Sh20,000 hii ni kwa mujibu ya kanuni ya mazingira. Tuwakumbusha watu kwa sababu adhabu hizi zilikuwepo tangu zamani.”

“Kanuni ya 45(1)ya  usimamizi wa taka ngumu, inaeleza atakayetupa uchafu wowote atapewa adhabu isipoungua Sh200,O00 kama mtu binafsi. Kama kampuni ni Sh5milioni,” amesema Heche.

Amewataka wamiliki wa mabasi kuwaeleza abiria kutotupa taka hovyo hasa vifungashio vya bidhaa mbalimbali ikiwemo korosho wanapomaliza kuvitumia badala yake waviweke katika utaratibu  ambao hautaathiri mazingira.

Share.

About Author

Leave A Reply