Thursday, July 18

Huduma zao zinasakwa wakiwa Afcon 2019

0


FAINALI za 32 za Afcon zimeshaanza huko Misri tangu juzi Ijumaa, ambapo wenyeji Misri walijipigia Zimbabwe na kuanza vyema kampeni yao ya kusaka ubingwa huo wa Afrika.

Kwenye mechi hiyo ilishuhudia mastaa kadhaa, akiwamo Mohamed Salah, aliyekuwa upande wa Misri ambao waliandikisha mwanzo mzuri katika mchakamchaka huo wa Afcon 2019.

Michuano hiyo inahusisha mastaa wengi sana, huku orodha yao wakiwa kibao wanasakwa na timu za huko Ulaya kwa ajili ya kuwasajili katika kipindi hiki cha uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Hii ndio orodha ya masupastaa wa nguvu waliopo kwenye Afcon 2019 ambao huduma zao zinasakwa usiku mchana na vigogo wa Ulaya kama vile Liverpool, Manchester United na Arsenal. Bila shaka, skauti wa klabu hizo na nyingine za Ulaya watakuwa huko Misri kufuatilia viwango vya mastaa hao.

Serge Aurier (Ivory Coast)

Beki huyo wa Ivory Coast, Serge Aurier sio chaguo la kwanza kwenye beki ya kulia ya Tottenham, hivyo anafikiria kutimkia kwingineko kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Kuna timu kibao zinahitaji huduma ya beki huyo mwenye uzoefu mkubwa kwenye soka, hasa ikizingatiwa kwamba huenda Spurs wakaamua kufanya mabadiliko kwenye kikosi chao katika dirisha hili kwa kuondoa basi ya wachezaji na Aurier anaweza kuwa mmoja wao.

Winga huyo anatarajiwa kuachana na FC Porto wakati mkataba wake utakapofika tamati katika kipindi hiki, licha ya kwamba msimu uliopita alifunga mabao 13 na kuasisti mara tisa kwenye kikosi hicho katika michuano yote. Brahimi, anahusishwa na klabu kibao za Ligi Kuu England zinazohitaji huduma yake ikiwamo Arsenal, Manchester United, Everton na Wolves. Bila ya shaka maskauti wa timu hiyo watakuwa huko Misri kwenda kumfuatilia winga huyo kuona kama wanaweza kumnasa.

Idrissa Gana Gueye (Senegal)

Kwenye dirisha la Januari, kiungo Idrissa Gueye alibaniwa nafasi ya kwenda kujiunga na Paris Saint-Germain, lakini katika dirisha hili la majira ya kiangazi bila ya shaka Msenegali huyo atajiandaa kuachana na Everton. PSG bado hawajakata tamaa katika kuisaka huduma ya kiungo huyo wa kati ambapo Gueye mwenyewe atahitaji kwenda kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, huduma ya kiungo huyo wa kati imekuwa ikiuliziwa pia na Man United ambao wamepanga kujiimarisha zaidi katika dirisha hili.

Kalidou Koulibaly (Senegal)

Beki wa kati, Kalidou Koulibaly amekuwa kwenye raha za klabu nyingi sana za Ulaya zinazosaka huduma yake. Kuanzia Chelsea, Manchester United na Liverpool zote zinahitaji saini ya beki huyo anayekipiga kwenye kikosi cha Napoli, ambaye huko kwenye Afcon 2019 atakuwa katika kikosi cha Senegal. Beki huyo anaweza kunaswa kwa ada ya Pauni 84 milioni na hiyo itaweka rekodi ya kuwa beki ghali zaidi duniani kama atanaswa katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Kiungo huyo wa Kinigeria anakipiga kwenye kikosi cha Leicester City huko katika Ligi Kuu England. Huduma yake imekuwa ikisakwa na timu nyingi za Ulaya na England ikiwamo Man United, ambao walitajwa sana kuwa na mpango wa kutaka huduma ya mchezaji huyo wa Super Eagle. Ndidi, aliyewahi kuichezea Genk, anayochezea Mtanzania Mbwana Samatta, ni miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye mikikimikiki ya Afcon 2019, ambao saini zao zinasakwa na klabu kibao kubwa za Ulaya.

Kipa, Onana alikuwa kwenye kikosi kile matata kabisa cha Ajax kwenye msimu uliopita kilichofika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa soka la Ulaya. Kiwango chake bora alichokionyesha akiwa golini huko Ajax kimezivutia timu nyingi zinazohaha kusaka huduma yake, ambapo vigogo kama Barcelona, Arsenal, Tottenham na hata West Ham wamekuwa wakipiga hesabu za kuipata huduma yake. Kuna kipindi Man United walihusishwa na kipa huyo wakitaka kumsajili baada ya kushindwa kumwelewa David De Gea.

Kiungo wa Atletico Madrid ya huko Hispania, Thomas Partey ni miongoni mwa wachezaji wanaozikosesha usingizi timu nyingi zinazohitaji huduma yake katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Partey amekuwa kwenye mipango ya timu nyingi ikiwamo Arsenal na Man United, lakini huko kwenye Afcon 2019 atakuwa ndani ya uzi wa Ghana, ambao ni moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa. ripoti zilizopo ni kwamba Partey ataruhusiwa na timu yake aondoka kama kutawekwa mezani dau la Pauni 43.5 milioni tu kutokana na kipengele kinavyobainisha kwenye mkataba wake.

Nicolas Pepe (Ivory Coast)

Wakali kama Dimitri Payet, Yohan Cabaye na Eden Hazard wote waliwahi kupita kwenye klab ya Likke, ambayo kwa sasa supastaa wao hatari ni Muivory Coast, Nicolas Pepe. Kwa hali ya mambo ilivyo kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Pepe haonekani kabisa kama anaweza kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho kutokana na ukweli kwamba timu nyingi zinahitaji huduma yake ikiwamo Man United inayohitaji winga mwenye kasi na uwezo wa kufunga katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya. Liverpool pia wanamtaka staa huyo na bila ya shaka itakuwa na skauti wake Afcon 2019.

Jean-Michael Seri (Ivory Coast)

Kiungo Jean-Michael Seri anatazamiwa kwenda kuifanya Afcon 2019 kuwa sehemu ya kutamba upya na kujikaribishia dili za maana mezani. Mwaka jana aligoma dili za kwenda kujiunga na Chelsea na Liverpool na kuamua kujiunga na Fulham, mahali ambako mambo hayakwenda vyema na timu hiyo kushuka daraja. Kutokana na hilo, bila ya shaka Seri atakuwa kwenye njia ya kutokea huko kwenye kikosi cha Fulham huku timu kibao zikihitaji saini yake aende akakamatie vilivyo kwenye kiungo ya kati. Seri ni mmoja wa mastaa wanaosakwa huko Afcon 2019, klabu kadhaa zikihitaji huduma zao kwa ajili ya msimu ujao. Huenda akaibukia Italia kwenye Serie.

Inaeleweka wazi kabisa kwamba, Tottenham itapitisha fagio kwenye kikosi chao majira haya na huenda kiungo wa Kenya, Victor Wanyama akawa mmoja wa wachezaji watakaofunguliwa mlango wa kutokea kwenye kikosi hicho. Kutokana na hilo, klabu nyingi za Ulaya zimeshafahamu kwamba Wanyama anaweza kufunguliwa mlango wa kutokea, hivyo ni wazi zitatuma skauti wao kwenda kumfuatilia kiungo huyo huko kwenye Afcon 2019 kuona ubora wake kabla ya kumnasa kwa ajili ya ligi ya msimu ujao. Kuna timu nyingi zinahitaji huduma ya kiungo huyo ikiwamo za Ligi Kuu England.

Wilfried Zaha (Ivory Coast)

Ni jambo la wazi kwamba Wilfried Zaha ana nafasi ndogo ya kuendelea kubaki Crystal Palace kutokana na kiwango cha soka lake kuwa kikubwa sana ukilinganisha na timu anayochezea.

Staa huyo alisema wazi kwamba anataka kuachana na timu hiyo kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi akitaka kwenda kujiunga na klabu kubwa.

Bila shaka kutakuwa na skauti kibao wa kutoka katika timu mbalimbali watakaokwenda Afcon 2019 kwenda kumfuatilia staa huyo ili kumng’oa kutoka Selhurst Park katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Man City wanamtaka, lakini Man United walikuwa wakipiga hesabu za kumrudisha kwenye kikosi chao huko Old Trafford.

Staa mwingine wa Ajax aliyecheza soka la kiwango cha juu sana msimu uliopita alikuwa Hakim Ziyech, ambaye naye atakuwapo huko kwenye Afcon 2019 akikitumikia kikosi cha Morocco. Staa huyo jina lake linatajwa sana kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi ambapo Arsenal wanatajwa kuwa na mpango wa kumsajili huku ikiwekwa bayana dau lake ni Pauni 25 milioni tu.

Ziyech kuna kipindi alihusishwa pia na Man United, lakini wachambuzi wa mambo ya soka na usajili wanadai kwamba staa huyo ana nafasi kubwa ya kwenda kujiunga na Arsenal, ambao hata yeye mwenyewe anapenda kwenda kuitumikia timu hiyo.

Mbwana Samatta (Tanzania)

Shughuli aliyofanya straika huyo wa Taifa Stars kwenye kikosi cha Genk huko Ubelgiji si ya mchezo. Mabao yake muhimu yameifanya timu hiyo kubeba ubingwa. Kutokana na hilo, Samatta amekuwa kwenye orodha ya wachezaji wanaosakwa na timu kibao kwenye dirisha hili ambapo kuna klabu kibao za England zinahitaji saini yake.

Kutokana na hali ilivyo, Samatta anaweza kuibukia kwenye Ligi Kuu England msimu ujao kutokana na Aston Villa kutajwa kuwa miongoni mwa timu zinazohitaji huduma yake matata.


Share.

About Author

Leave A Reply