Saturday, August 24

Hoteli zaidi ya 50, kupewa mafunzo ya usalama wa chakula

0


By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Watoa huduma katika hoteli za hadhi ya juu nchini wanatarajiwa kupewa mafunzo kuhusu usalama wa chakula ili kuinua kiwango cha huduma za hoteli kuwa cha kimataifa.

Mafunzo hayo ambayo yameshirikisha Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania TFDA pamoja na Wizara ya Afya, yatatolewa kwa zaidi ya hoteli 50 za jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana Mei 25, mwaka 2019, Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Mazouk Production, Dk Salum Kihemba alisema mafunzo hayo yaliyopangwa kufanyika Julai 19 mwaka 2019, yamelenga kuboresha sekta ya huduma za hoteli kwa viwango vyote.

Kihemba ambaye pia ni mtaalamu wa sheria na uchumi wa fedha, alisema licha ya walengwa kuwa hoteli zenye hadhi, Wenye kuhitaji mafunzo na waandaaji wa vyakula katika sehemu mbalimbali watajumuishwa.

“Tunataka mtalii akija apate huduma sawasawa na ile anayoipata katika hoteli zingine kwenye nchi zilizoendelea, tumegundua katika hoteli zetu kila mtu anafanya utaratibu wake wa ndani kuhakikisha usalama, usafi na ubora wa chakula hoteli zote hazina watu ambao wana hiyo taaluma.”

Amesema nchi kama Marekani mama mjamzito, mzee, mtoto chini ya miaka mitano au wenye upungufu wa kinga wana namna yao ya kuandaliwa chakula.

“Hapa kwetu hakuna huo utaalamu na ndiyo maana tumeona tuwashirikishe TFDA ingawa sisi hatuingizi chakula ila tumewahusisha wao pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ndiyo maana tumeweza kuzungumza na Wizara ya Afya pia ili kuona utaratibu unaokubalika na endelevu kwa kudhibiti vitu kama hivi,” alisema Dk Kihemba.

Alisema kutokana na utaratibu wa kutoa mafunzo, imekuwa sababu kwa nchi hizo kutokuwa na magonjwa mbalimbali yatokanayo na uchafu au sumu katika chakula (food poison).

“Tunataka kuingiza uwepo wa utaratibu stahiki katika usambazaji na utoaji wa huduma bora ya chakula kwa kweli Serikali imefanya kazi kubwa katika kudhibiti pamoja na hivyo ipo haja kwa hoteli na wote wanaohusika na chakula kufanya mafunzo ili kulinda afya ya jamii,” amesema.

Aidha Dk Kihemba amesema mafunzo hayo yatakayofanyika Julai 19 katika hoteli ya Hyatt Regency – The Kilimanjaro, kiingilio itakuwa Sh230,000 yatafanyika pia katika mikoa ya Arusha na Zanzibar.

Share.

About Author

Leave A Reply