Saturday, August 17

HOFU YA KIMBUNGA KENNETH: Mkakati kabambe wa uokoaji

0


By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha madhara ya Kimbunga Kenneth yanadhibitiwa, Serikali, taasisi zake na mashirika mbalimbali yametangaza mikakati uokoaji ikiwamo helikopta na vikosi ambavyo vimesambazwa katika maeneo mbalimbali ya Mtwara na Lindi.

Jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu), Jenista Mhagama alisema Kamati ya Maafa ya Taifa imeandaa helikopita zitakazotumika katika kukabiliana na changamoto ya kimbunga hicho kilichotarajiwa kutokea kuanzia usiku wa kuamkia leo.

Waziri Mhagama alisema pamoja na hatua hiyo, shughuli za biashara, uvuvi zimezuiliwa, shule zimefungwa, usafiri wa anga, barabara na vyombo vya usafiri majini umesitishwa kwa muda kwaa watu waishio maeneo ya Pwani ya ukanda huo.

“Tumehakikisha tahadhari zote katika menejimenti ya maafa zimekuwa tayari, ili wakati wowote ikitokea tusaidie Watanzania, tuwaokoe. Ziko taasisi nyingi tunafanya kazi nazo, tumeshaanza kuangalia mahitaji yanayotakiwa dawa, huduma ya kwanza na helikopita za uokoaji,” alisema Waziri Mhagama jana kupitia mahojiano yake na Kituo cha Channel Ten.

Alisema Kamati ya Maafa inaendesha kampeni ya utoaji wa elimu ngazi ya vijiji hadi wilaya.

“Kinachotakiwa kwa sasa ni umoja kama Watanzania, tuombe Mungu na tusaidiane kutoa taarifa na msaada kwa masilahi ya Taifa, tumeshaandaa baadhi ya hospitali katika mikoa hiyo kwa ajili ya utoaji wa huduma endapo kimbunga hicho kitatokea,” alisema.

Usafiri wa baharini Zanzibar

Jana mchana, Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA) ilisitisha shughuli za usafiri kutokana uwepo wa taarifa za kutokea kimbunga hicho.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na kaimu mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Ramadhan Hussein imesema wamelazimika kusitisha shughuli za safari kwa vyombo vyote baharini hadi pale taarifa zaidi za mamlaka ya hali ya hewa zitakapotolewa.

“Kwa kuwa tumepata taarifa za kuwepo kimbunga nchini Tanzania nasi kama sehemu ya Tanzania, tumeona kuna umuhimu wa kusitisha safari zetu,” alisema.

Alisema mbali ya hatua hiyo, alitoa wito kwa wavuvi kusitisha shughuli zao hadi hali ya utulivu itakaporejea ili kujinusuru mapema na janga la kimbunga ambalo linaweza kutokea.

Hussein alitoa wito kwa wananchi wote waliopo maeneo ya karibu na Bahari ya Hindi kufuatilia pamoja na kufuata maagizo ya mamlaka hiyo pamoja na Hali ya Hewa.

Wadau wengine ambao wapo katika mikoa hiyo tayari kutoa msaada ni Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) ambalo limesema vikosi vyake Lindi na Mtwara vimekamilisha maandalizi ya uokoaji endapo lolote litatokea.

Ofisa Habari wa TRCS, Godfrida Jola alisema jana kuwa timu ya watu 50 tayari ipo kwenye mikoa hiyo kutoa huduma ya kwanza ikiwa kimbunga hicho kitaleta madhara yoyote.

Akizungumza kwa simu jana, Godfrida alisema timu hiyo imegawanywa katika makundi ya watu 10 ambao watapita kwenye mikusanyiko ya watu kuona hali halisi na kujua mahitaji muhimu yatakayojitokeza.

Alisema tayari gari la huduma ya kwanza limeshawasili Mtwara kwa ajili ya kukabiliana na athari endapo zitatokea.

Alisema ni muhimu watu walio kwenye maeneo hatarishi kukaa sehemu salama.

Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Tumaini Msowoya na Haji Mtumwa

Share.

About Author

Leave A Reply